Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema ni jambo muhimu kwa viongozi wa Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazojitegemea kupatiwa mafunzo yatakayowajengea uwelewa mpana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya wakuu wa Taasisi zinazojitegemea za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Tume ya Uchaguzi Maisara Zanzibar.
Amesema mafunzo hayo kwa kiasi kikubwa yatawasaidia katika kutekeleza majukumu yao, kutambua muelekeo sahihi wa Serikali sambamba na kujengewa uwezo wa kuziongoza Taasisi na Idara zao kwa weledi, ufanisi na tija.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ni hatua nzuri katika kufikia malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayoendelea kusisistiza umuhimu wa kujenga rasilimali watu wenye ujuzi, madili, weledi na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kiutawala, kiuchumi na kiteknolojia.
Aidha, amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya mifumo ya kazi, matumizi ya Teknoloji na uwajibikaji wa Umma ni dhahiri kwamba mafunzo endelevu kwa watumishi wa umma na viongozi wa ngazi za juu si hiari bali ni hitaji la msingi katika kujenga utwala bora na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa mafuzo hayo yanawapa viongozi fursa ya kujitathmini, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za uongozi na kuimarisha maamuzi yenye tija kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo Mhe. Hemed ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kushiriki kikamilifu na kujifunza kwa umakini ili kuweza kuwa mabolozi wazuri wa mabadiliko chanya katika Taasisi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA ) Dkt. Abduhamid Yahya Mzee amesema Chuo cha IPA kitaendelea na mpango wake wa kutoa mafunzo kwa watumishi na viongozi wa Taasisi mbali mbali ili kuweza kukumbushana, kujadili na kubadilishana uzowefu katika utendaji wa kazi za kila siku.
Dkt. Abdulhamid amefahamisha kuwa Mafuzo hayo yanalenga kuwapatia taaluma viongozi juu ya namna bora ya kuongoza kwa weledi, ufanisi na kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji wao wanaowaongoza ili kufikia adhma ya kuwa viongozi wabunifu, wenye busara na hekima kwenye Taasisi zau wanazoziongoza.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Balozi, Mhandisi Zena Ahmed Said amesema mafunzo hayo yatakuwa endelevu ambayo yanalenga kuwakumbusha viongozi wa Umma kuwajibika ipasavyo kwa uadilifu na nidhamu katika majukumu yao.
Balozi Muhandisi Zena amesema katika mafunzo hayo mada mbali mbali zitawasilishwa ikiwemo Uongozi Bora, Itifaki na Uongozi, Uongozi wa Kimkakati na jukumu la usalama, Maadili na Usiri katika sehemu za kazi.
.jpeg)



No comments:
Post a Comment