Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatoa fursa muhimu ya kupatiwa ufumbuzi wa haraka changamoto zinazojitokeza katika masuala ya pamoja ya Muungano.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, aliyeambatana na watendaji wakuu wa Wizara hiyo, waliofika Ikulu, Zanzibar, leo tarehe 18 Februari 2026 kwa ajili ya kujitambulisha.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inaridhishwa na mwendelezo wa vikao vya pamoja vinavyolenga kutatua changamoto za masuala ya Muungano, na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa utaratibu bora zaidi utakaoinufaisha Zanzibar, hususan katika suala la upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameishauri Wizara ya Fedha kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha ushirikiano wa kifedha na kiuchumi, ili kuhakikisha masuala ya Muungano yanashughulikiwa kwa ufanisi, uwazi na kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wa kiwango cha juu na kufanya kazi kwa pamoja katika kuzitumia kikamilifu fursa za kifedha na kiuchumi, kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania Bara








No comments:
Post a Comment