Sunday, February 08, 2026

HESLB YATUZWA TAASISI KINARA MATUMIZI YA MIFUMO KIDIGITALI










Dar es salaam, Februari 08, 2026

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angela Kairuki ameipongeza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuwa taasisi kinara na ya kidigitali katika utoaji wa huduma na utendaji wa kila siku na kuikabidhi tuzo ya kutambua mchango wake katika matumizi ya anwani za makazi.

Waziri Kairuki ambaye amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 08, 2026) alipotembelea banda la HESLB kwenye Maonesho yaliyoenda sambamba na Mkutano wa Kimataifa wa Mwaka wa Anwani za Makazi na Teknolojia ya Huduma za Posta (TACPA) yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Waziri Kairuki ameiagiza HESLB kuongeza kasi ya makusanyo ya mikopo ya wanafunzi ili kuongeza mchango wake katika utoaji wa mikopo ya wanafunzi ambao wanaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

“Ningependa kuona kiasi cha makusanyo kinaongezeka … hii itasaidia kupunguza mzigo kwa Serikali na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kujiunga na elimu ya juu”, amesema Mhe. Kairuki.

Licha ya maonesho, HESLB pia ilishiriki katika kongamano kuhusu Nafasi ya Anwani za Makazi katika ukuaji wa Sekta mbalimbali na kisha kuendelea kwenye majadiliano kuhusu jinsi ambayo HESLB imetumia anwani za makazi na changamoto zilizojitokeza wakati wa maombi ya mikopo kwa mwaka 2025/2026 kuanzia Julai 15, hadi Septemba 15, 2025.

HESLB ni miongoni mwa taasisi zinazotumia anwani ya makazi hususan katika huduma ya maombi ya mikopo kwa wanafunzi kikiwa ni kipengele muhimu kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026 ambacho kimewekwa kuwa ni moja ya taarifa ya msingi inayohitajika kutoka kwa mwombaji na wazazi wake kabla ya kumpangia mkopo stahiki.  

Washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wametumia jukwaa hilo la siku nne kuanzia Februari 5 hadi 8, 2026 ili kujadili kwa pamoja mafanikio, changamoto na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau kwa lengo la kuboresha eneo la anwani za makazi na teknolojia ya huduma za Posta likiwa na kauli mbiu isemayo, “Anwani Mahiri na Ubunifu wa Huduma za Posta kwa Ukuaji Jumuishi.

Mkutano na Kongamano hilo lmefanyika kwa mara ya pili na kujumuisha washiriki 1, 000 kutoka nchi mwenyeji Tanzania na wageni kutoka Guinea, Burkina Faso, Korea ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Malawi.

No comments:

RAIS SAMIA AFUNGUA SOKO LA KISASA KARIAKOO LILILOGHARIMU BILIONI 28, SASA BIASHARA SAA 24

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Sok...