Katibu Mkuu Wizara ya maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo na Visay Uplenchwar wa Kampuni ya Megha Engineering Infrastructures Ltd akisaini Mikataba ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka kijiji cha Solwa Shinyanga na kupeleka maji Nzega.
Picha ya pamoja Meza kuu pamoja na baadhi ya Wabunge wa Tabora.
Mbunge wa Nzega Hussein Bashe akimsalimia waziri wa Maji na Umwagiliaji Eng. Lwenge
Waziri wa maji na Umwagiliaji Eng. Gerson Lwenge akipokewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora wakati alipowasiri katika viwanja vya Furahisha Tabora.
Mbunge wa Sikonge Joseph Kakunda akimpa mkono Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Na: Athumani Shariff
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo amesaini kandarasi zenye thamani ya dola za Marekani Milioni 268.35 ambazo ni zaidi ya Shilingi bilioni 600 za Tanzania mjini Tabora kwa mkopo wa benki ya Exim ya nchini India kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoa Ziwa Victoria na kupeleka katika Manispaa ya Tabora na Halmashauri za Igunga, Uyui, Shinyanga Vijijini na Nzega.
Utekelezaji wa mradi ni wa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ya Mradi ilikuwa kufanya usanifu na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi, kazi ambayo ilifanywa na Kampuni ya WAPCOS Ltd ya India na ilikamilika mwezi Desemba 2015.
Awamu ya pili ni ujenzi wa mradi ambao umegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza itaanzia Kijiji cha Solwa (kilichopo Wilaya ya Shinyanga Vijijini) hadi Mji wa Nzega, ujenzi utafanywa na Kampuni ya Megha Engineering Infrastructures Ltd ya India. Sehemu ya Pili inaanzia Mjini Nzega mjini hadi Manispaa ya Tabora kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, ujenzi utafanywa na Kampuni ya L&T ikishirikiana na kampuni ya Shriram zote kutoka India.
Sehemu ya tatu inaanzia Nzega mjini hadi Igunga mjini, ujenzi utafanywa na Kampuni ya Afcons ikishirikiana na kampuni ya SMC zote kutoka India. Usimamizi wa mradi unafanywa na Kampuni ya WAPCOS Ltd ya India.
Katika hotuba yake Profesa Mkumbo alisema wakandarsi hao wameanza kazi leo mara baada ya kusaini mikataba. “Wakandarasi wanaanza maandalizi yao leo na kazi za ujenzi zitaanza mwezi Mei 2017 na muda wa kukamilisha mradi utakuwa baada ya miezi 30”. Alisema Prof. Mkumbo.
Kwa upande mwengine Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge, alisema uchumi wa Viwanda hauwezekani bila uhakika wa maji, hivyo Wizara yake itasimamia kwa kina juu ya uharaka wa mradi huo ili kuhakikisha sera na dira ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda inafanikiwa.
“Nitahakikisha Wakandarsi hawa wanamaliza kazi kwa ubora na haraka kabla ya muda ili kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika azma yake ya Tanzania ya viwanda, kwasababu hakuna viwanda bila maji ya uhakika”, alisema Waziri Lwenge.
Na serikali ya awmu ya tano ni serikali ya uwazi ndiyo maana nimeagiza zoezi la kusaidi ujenzi wa miradi hii ifanyike hadharani ili ninyi wananchi wenye miradi yenu muone, sasa mushirikiane na wakandari hao na muwe walinzi wa vifaa ili kazi waifanye kwa haraka. Isitokee baadhi ya wananchi wasio waaminifu kuhujumu vifaa vya ujenzi mambo ambayo yatachelewesha mradi.” Alisisitiza Waziri Lwenge.
Pia Lwenge aliwataka wakazi wa Tabora na maeneo mengine nchini watunze vyanzo vya maji ili miradi hii ya maji iwe endelevu. Alisisitiza kuwa sheria inakataza shughuli zote za kibinadamu kufanywa ndani ya mita sitini kutoka kwenye chanzo cha maji.
“Tujiepushe kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya mita 60, ili tuwe na uhakika wa maji, tupande miti na kutunza mazingira yetu” alisema mhandisi Lwenge.
Kwa upande wao wabunge wa Tabora ambao mradi utapita katika maeneo ya majimbo yao wameishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yao ya muda mrefu ya kuwaondolea kero ya uhaba wa maji katika maeneo yao.
Akieleza umuhimu wa mradi huo, Mbunge wa Sikonge Joseph Kakunda alisema mradi huu ni muhimu na mkombozi kwakuwa hamna vyanzo vya maji vya uhakika katika maeneo mengi ya Mkoa wa Tabora.
Mbunge Hussein Bashe aliomba wakandarasi wa ndani nao wafikiriwe ili waweze kupata baadhi ya kazi ndogondogo (sub-contracts) ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa ndani na kuwajengea uwezo wakandarasi wetu nchini.
Akieleza mafanikio ya mradi Profesa Mkumbo alisema kuwa, mradi ukikamilika upatikanaji wa maji katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Uyui pamoja na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, unatarajiwa kuongezeka kufikia asilimia 100 na wakazi zaidi ya milioni 1.1 watapata huduma ya maji safi na salama.
Pia alisema huduma bora ya maji itakayopatikana itachangia katika kuinua uchumi kupitia maendeleo ya sekta nyingine zinazotegemea maji kama Viwanda,Elimu, Utalii pamoja na kuimarisha huduma za afya wa wakazi wa maeneo hayo.
Comments