Wednesday, September 26, 2012

CHIKAWE ALONGA UMOJA WA MATAIFA


Waziri wa Katiba na Masuala ya Sheria, Mhe. Mathias Chikawe ( Mb ) akipitia kwa mara ya mwisho hotuba yake kabla ya kuisoma, wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukajadili Utawala wa Sheria katika Ngazi ya Kimataifa na Kitaifa, katika hotuba yake katika mkutano huo ambao ulifunguliwa na Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, na kuhutubiwa na Viongozi wakuu wa nchi na serikali wakiwamo Mawaziri kutoka nchi 80, alielezea namna ambavyo Jamhuri ya Muungano imekuwa ikizingatia utawala wa sherika katika ngazi ya taifa, kanda na kimataifa na akaelezea pia mchakato unaoendelea wa maandalizi ya Katiba mpya. wengine katika picha kuanzisha kulia ni Mhe. Abubakari khamisi Bakari,(Mb) Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe, Musa Hassan Mussa ( Mb) kutoka Zanzibar na waliokaa nyuma ni wataalam wa sheria.

Mhe. Mathias Chikawe ( Mb) akihutubia Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukijadili ajenda ya Utawala wa Sheria katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa. Mkutano huo wa Siku Moja ulifanyika siku ya Jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. 

Na Mwandishi Maalum 

Waziri wa Katiba na Masuala ya Sheria Mathias Chikawe ( Mb) amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejidhatiti ipasavyo katika utekelezaji na uzingatiaji wa utawala wa sheria kuanzia ngazi ya taifa, kanda na kimataifa. Chikawe ameyasema hayo jana jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, katika Mkutano wa kilele ambao ajenda yake kuu ilikuwa ni Utawala wa Sheria kitaifa na Kimataifa”. 

Mkutano huo ambao umeandaliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki Moon, umehudhuriwa na kuhutubiwa na viongozi wakuu wa nchi na serikali na mawaziri zaidi ya 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa. 

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa kuandaa mkutano wa aina hii ambao ulijikita katika kuzungumzia utawala wa sheria kama kiungo muhimu kati ya ngazi ya kitaifa na kimataifa na ukuaji wa uchumi, maendeleo endelevu na kuondoa umaskini na njaa Aidha mkutano huo pia umetoa fursa kwa nchi kuelezea namna gani zimekuwa zikizingatia au kutekeleza utawala huo katika ngazi ya kimataifa na kimataifa.

 Mkutano huu umefanyika siku moja, kabla ya kuanza kwa majadiliano ya Mkutano wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mkutano utakaofunguliwa leo siku ya Jumanne, utahutubiwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa Marekani Barack Obama. 

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu wa 67 unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe(Mb) akimwakilisha Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete. 

Waziri Mathias Chikawe ni miongoni wa wajumbe wanaohudhuria mkutano huu akiwamo pia Mhe. Abubakari Khamis Bakali (Mb), Waziri wa Katiba na Masuala ya Sheria kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Vita Kawawa ( Mb) na Mhe. Musa Hassan Musa ( Mb) kutoka Zanzibar Akizungumzia utawala wa sheria katika ngazi ya kitaifa, Waziri Mathias Chikawe amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, utawala wa sheria ni sehemu ya makubaliano ya kijamii kati ya taifa na mtu binafsi.

 “ Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imekuwa nguzo muhimu katika kutoa mwongozo na kipimo cha utawala bora. Na kwa sababu hiyo misingi ya usawa mbele ya sheria, uwajibikaji kwa sheria na mgawayo wa madaraka vimezingatiwa katika utawala wa sheria” akasema na kuongeza “ Kwa kuzingatia kwamba Katiba inatokana na wananchi na inazingatia kile ambacho wananchi wanataka, Tanzania hivi sasa iko kazi zoezi linalohusisha kila mtu kupitia Katiba ya sasa kwa alengo la kuanda katiba mpya baada ya Katiba ya sasa kuitumikia Tanzania kwa miaka 50 iliyopita”.

 Ameeleza. Aidha Waziri Chikawe amesema Katiba ya Tanzania pia imetoa nafasi ya kuanzishwa kwa taasisi za kitaifa zenye wajibu wa kuhakikisha kwamba utawala wa sheria siyo tu unafuatwa lakini pia haki za wananchi zinalindwa Akabainisha kwamba baadhi ya taasisi za aina hiyo ni Kamisheni ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, taasisi ambayo kwa miaka mingi imeendelea kufanya kazi nzuri. 

Akaongeza kwamba uzingatiaji wa misingi ya ulinzi na uhifadhi wa haki za binadamu, fursa ya kupata haki na uasawa, utawala bora na utawala wa sheria nchini ni mambo ambayo yamezingatiwa vema katika Dira ya taifa ya mwaka 2025 na Mpango wa Taifa wa Kukuza uchumi na Kupunguza Umaskini.

 Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Utawala wa Sheria amesema, uimarishaji wa mfumo wa sheria ni moja yamambo ambayo yamepewa kipaumbele katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Na kwamba serikali imefanya jitihada za makusudi za kuongeza idadi ya majaji, mahakimu, ujenzi wa mahakama mpya na kuzikarabati za zamani. 

 Akaeleza pia kwamba kumekuwa na mikakati ya kuboresha huduma za mahakama kwa kuanzisha huduma itakayojulikana kama tele justice. Aidha akauelezea umma huo wa Umoja wa mataifa, kwamba Tanzania imejipanga kupambana kikamilifu na rushwa ili kuwa na jamii huru. Awali akufunguaa mkutano huo ambao mwishoni ulipitisha Andiko, Katibu Mkuu Ban Ki Moon alitoa mwito kwa jumuia kushirikiana na kwa kutumia sheria ya kimataifa, kutatua migogoro kwa njia ya zamani na kuhakikisha kwamba mgogoro hiyo haitokei tena. 

Aidha Katibu Mkuu amezitaka nchi kuimarisha utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya polisi na kuimarisha idara ya mahakama hususani katika nchi zile ambao hali ya amani ni tete na zimekuwa zikikumbwa na migogoro. Kwa upande wake, Rais wa Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa Bw. Vuk Jeremic ameonya dhidi ya kuona sheria ya kimataifa kama nyenye umuhimu mdogo na inamadhara kwa uendeshaji wa masuala ya dunia Akasisitiza kwamba kama nchi na watawala watakuwa madhubuti na kuzingatia utawala wa sheria ni wazi hakuta kuwapo na ushawishi wa kukimbilia vita. 

Akasisitiza umuhimu wa uwepo wa Makama ya Makosa ya Jinai (ICC) na kuzitaka nchi ambazoa hazijaitambua mahaka hiyo au kuiona kama si sehemu ya Umoja wa Mataifa kuachana na dhana hiyo Akasema kazi ya ICC ni pamoja na kuhakikisha kwamba haki inatendekea kwa kuwafikisha mbele ya mahakama hiyo watuhumiwa wa makosa ya jinai na kuzuia kutoa jirudia kwa mauaji ya kimbari. 

 Aidha mkutano huo pia ulihutubiwa na viongozi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama vile Kamisheni ya Haki za Binadamu, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ) ICJ Bw Petro Tomka ambaye alibainisha kwamba ni nchi 67 tu kati ya Nchi 193 za Umoja wa Mataifa, sawa na asilimia 34 ikiwa ni pamoja na mwanachama mmoja tu wa Baraza kuu la Usalama ambazo zimeikubali na kuitambua ICJ.

No comments: