JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MTIHANI WA KUMALIZA
ELIMU YA MSINGI MWAKA 2012
Ndugu
wananchi,
Mtihani
wa Kumaliza Elimu ya Msingi Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 na 20
Septemba, 2012. Jumla ya wanafunzi 894,881 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambapo wavulana ni 426,285 sawa na asilimia 47.64 na wasichana ni 468,596 sawa na asilimia 52.36. Aidha, kati
ya wanafunzi hao, wapo wanafunzi 874,379 watakaofanya
mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 20,502 watafanya kwa
lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia kujifunzia. Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya
mtihani ni 92 wakiwemo wavulana 53 na wasichana 39. Watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji
maandishi makubwa ni 495, kati
yao wavulana ni 238 na wasichana ni 257.
Mtihani
huu utafanyika kwa mara ya kwanza kwa kutumia teknolojia mpya ya ‘Optical
Mark Reader’ (OMR), ambapo watahiniwa watatumia fomu maalum za OMR kujibia
mtihani na majibu yao yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta. Masomo yatakayotahiniwa katika mtihani huo ni
Kiswahili, English Language, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Ndugu
wananchi,
Maandalizi
yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa
karatasi za mitihani, kusambazwa kwa fomu maalum za kujibia mtihani na nyaraka zote zinazohusu
mtihani huo. Mafunzo maalum kwa ajili ya matumizi ya fomu za OMR yamefanyika
kwa lengo la kuwaandaa watahiniwa, wasimamizi pamoja na viongozi wa elimu
katika ngazi mbalimbali ili waweze kutumia ipasavyo teknolojia hiyo.
Ndugu wananchi,
Mtihani
wa Kumaliza Elimu ya Msingi ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa
kuwa unahitimisha ngazi ya Elimu ya Msingi na kufungua milango kwa ajili ya
elimu ya sekondari. Hivyo, matokeo ya mtihani
huu hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Elimu ya Sekondari. Kwa
kuzingatia umuhimu wa mtihani huo, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa
Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani
zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa salama na tulivu na kuzuia
mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.
Napenda
pia kutoa wito kwa wasimamizi wa mitihani kufanya kazi yao ya kusimamia kwa
umakini na uadilifu wa hali ya juu. Wapo
baadhi ya wasimamizi ambao wamekuwa wakishiriki katika kuwasaidia watahiniwa
kufanya udanganyifu kwenye mitihani. Napenda
kuwaasa tena wasimamizi kujiepusha na vitendo hivyo vya udanganyifu kwani
serikali haitasita kuchukulia hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika
kukiuka taratibu za mitihani.
Kwa upande
wa wanafunzi watakaofanya mtihani mwaka huu, ninaamini kuwa walimu wamewaandaa
vizuri katika kipindi chote cha miaka saba ya Elimu ya Msingi. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mtaufanya
mtihani huo kwa utulivu na kuzingatia taratibu zote za mitihani ili matokeo ya
mtihani yaoneshe uwezo wenu halisi kulingana na maarifa na ujuzi mliopata
katika Elimu ya Msingi. Serikali
inawaasa wanafunzi wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu katika
mtihani kwani watakaobainika watafutiwa matokeo yao yote ya mtihani.
Ndugu wananchi,
Natoa
wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba mtihani huo
unafanyika kwa amani na utulivu wa
kutosha bila usumbufu unaoweza kusababishwa na shughuli za kijamii hasa katika
maeneo ya jirani na shule.
Mwisho,
napenda kuwaasa tena wanafunzi, walimu na wananchi wote kwa ujumla kujiepusha
na vitendo vya udanganyifu wa aina yoyote katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya
Msingi. Nawaomba pia raia wema wasisite kutoa taarifa katika vyombo husika
pindi wanapoona au kuhisi mtu au kikundi cha watu kinajihusisha na udanganyifu
wa aina yoyote katika mtihani huo.
Nawatakia
watahiniwa wote heri na fanaka katika mtihani utakaofanyika tarehe 19 na
20 Septemba, 2012.
MHESHIMIWA PHILIPO AUGUSTINO MULUGO (MB)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
15
SEPTEMBA, 2012
No comments:
Post a Comment