Thursday, April 16, 2026

TANZANIA NA BRAZIL ZAJIZATITI KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA









Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Pili wa Mashauriano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Brazili uliofanyika jijini Brasilia, Brazili Aprili 15, 2026. 

Ujumbe wa Brazili katika mkutano huo uliongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Balozi Sobral Duerte Carlos Sergio Sobral Duerte. 

Katika Mkutano huo, Tanzania na Brazili zimejadili na kukubaliana mikakati mbalimbali ya kukuza uhusiano na Ushirikiano wa Kidiplomasia baina ya Tanzania na Brazili katika sekta mbalimbali. 

Baadhi ya sekta hizo ni pamoja na umuhimu wa viongozi wa nchi hizi mbili kuendelea kutembeleana na kubadilisha mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano ya uwili na kimataifa; Kukuza Ushirikiano katika sekta ya elimu na mafunzo ambapo Brazili itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Tanzania.

Pia kukuza ushirikiano katika sekta ya kilimo na ufugaji hususan katika matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji; pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kwa kukuza viwango vya biashara, uwekezaji na utalii baina ya nchi hizi mbili. 

Aidha, Tanzania na Brazili zimekubaliana kukamilisha majadiliano ya rasimu za makubaliano ya ushirikiano katika sekta husika ili ziweze kusainiwa na utekelezaji wake uanze mara moja.

Vilevile, Tanzania na Brazili zimebadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa pande zote, ikiwemo athari za migogoro ya kisiasa na vita ulimwenguni, mchakato wa Mageuzi ya Mifumo Ulimwenguni kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

No comments:

Makamu wa Rais wa Zimbabwe akutana na CP Kaganda kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Kembo Mohadi, amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo, Kamishna wa Po...