Thursday, April 23, 2026

UJUMBE WA MAAFISA KUTOKA CHUO CHA ULINZI CHA TAIFA MISRI WATEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA TANZANIA









Leo, tarehe 23/04/2026 Makumbusho ya Taifa la Tanzania imepokea ugeni maalum kutoka Chuo cha Kijeshi Misri (Egypt War College) walioko katika ziara ya mafunzo.

Ujumbe huo uliongozwa na Meja Jenerali Mohamed Yehia Zakaria Hassan akiambatana na Brigedia Jenerali Islam Sayed Bakry El-Sayed, huku kwa upande wa mwenyeji wao kutoka Tanzania wakiongozwa na Brigedia Jeneral Kamanda Makanya Erassy kutoka JWTZ Tanzania.

Wageni hao walipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Bi. Pendo Gondwe, ambaye aliwakaribisha na kuwapatia maelezo kuhusu dhima ya taasisi hiyo ya Kimkakati katika kuhifadhi, kulinda na kuendeleza urithi wa historia na utamaduni wa Taifa.

Ujumbe huo uliokuwa na lengo la kujifunza ulipata fursa ya kutembelea na kujifunza historia ya Tanzania kupitia vivutio mbalimbali vilivyopo katika Makumbusho, ikiwemo mabaki ya kihistoria, tamaduni za jamii mbalimbali pamoja na hatua za maendeleo ya taifa. Wageni hao walionesha kuvutiwa na ubora wa maonesho na namna historia ya Tanzania inavyoendelea kuhifadhiwa na kuwasilishwa kwa ufanisi.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, kiongozi wa ujumbe, Meja Jenerali Mohamed Yehia Zakaria Hassan, alieleza kufurahishwa kwake na kiwango cha maonesho hayo akisema, “ Maonesho ni bora sana na nimefurahishwa kuona mwendelezo wa historia ukiendelea kukua na kuendelezwa"* 

Ziara hiyo ni sehemu ya programu ya mafunzo kwa wanafunzi wa Egypt War College, yenye lengo la kuwajengea uelewa mpana kuhusu historia, utamaduni na mifumo ya kijamii ya mataifa rafiki, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kidiplomasia kati ya Tanzania na Misri.

No comments:

UJUMBE WA MAAFISA KUTOKA CHUO CHA ULINZI CHA TAIFA MISRI WATEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA TANZANIA

Leo, tarehe 23/04/2026 Makumbusho ya Taifa la Tanzania imepokea ugeni maalum kutoka Chuo cha Kijeshi Misri (Egypt War College) walioko katik...