Friday, April 24, 2026

🏗️ MASASI COMMERCIAL COMPLEX YAKABIDHIWA RASMI









Mradi wa Masasi Commercial Complex umekabidhiwa rasmi, ukiwa ni alama ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya kisasa yenye kuzingatia ubora na thamani kwa jamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi, Omari Malalamangi, aliipongeza timu ya ujenzi kwa kazi kubwa waliyoifanya licha ya changamoto ya maji wakati wa uchimbaji wa msingi. 

Alisisitiza kuwa kujituma kwao kumezaa matokeo bora—jengo lenye hadhi linalovutia na kupongezwa na wengi.

Mradi huu umeacha alama chanya kwa jamii, ukitoa ajira kwa wakazi wa Masasi na kunufaisha sekta mbalimbali zikiwemo huduma za maji, umeme, mama lishe pamoja na wauzaji wa vifaa vya ujenzi.

Kwa upande wake, Meneja Usimamizi wa Miradi NHC, Grace Musita, alieleza kuwa ujenzi umefuata taratibu zote za kitaalamu, huku vipimo vya vifaa kama nondo, kokoto na tofali vikifanyika katika maabara ya Mtwara. 

Alibainisha kuwa kila hatua ya ujenzi ilisimamiwa kwa ukaribu na wataalamu ili kuhakikisha ubora unazingatiwa kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.

Aidha, mradi umefungua fursa kwa wafanyabiashara wa ndani, ambapo baadhi ya kazi kama uwekaji wa milango ya mbao na tiles zilifanywa na mafundi wazawa wa Masasi.

Musita alimshukuru Mkurugenzi Mkuu pamoja na Menejimenti ya NHC kwa ushirikiano uliowezesha kukamilika kwa mradi huu kwa mafanikio.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Madaraka, Kata ya Jida, alieleza furaha yake akisema ujio wa jengo hili umeubadilisha mtaa huo na kuongeza uhai wa shughuli za kijamii na kiuchumi, huku ajira ndogo ndogo zilizotolewa zikichochea vijana wengi kujikwamua kiuchumi.

Hafla ya makabidhiano ilihitimishwa kwa kukata keki, kuashiria rasmi kuwa Masasi Commercial Complex ipo tayari kutumika.

#NHC #MasasiComplex #UjenziBora #MaendeleoYaJamii #Tanzania

No comments:

🏗️ MASASI COMMERCIAL COMPLEX YAKABIDHIWA RASMI

Mradi wa Masasi Commercial Complex umekabidhiwa rasmi, ukiwa ni alama ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya kisasa yenye kuzingatia ubor...