Taifa Gesi haitapandisha bei ya gesi ya majumbani (LPG) licha ya ongezeko la takribani asilimia 43 ya bei ya gesi hiyo duniani. Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kuendeleza upatikanaji nafuu wa nishati hiyo pamoja na kupunguza za athari za mabadiliko ya soko la kimataifa kwa wateja wake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Taifa Gas imeeleza kuwa soko la kimataifa la gesi ya kupikia limekumbwa na ongezeko kubwa la bei katika wiki za hivi karibuni na hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama za ununuzi katika minyororo ya ugavi na usambazaji duniani.
Alieleza kuwa katika wiki za hivi karibuni, soko la kimataifa la gesi ya kupikia limekumbwa na ongezeko kubwa la bei, hali iliyosababisha kupanda kwa gharama katika minyororo ya ugavi na usambazaji duniani.
“Katika mazingira haya ya sasa, tunayo dhamira ya dhati ya kuwasaidia wateja wetu kwa kubeba athari za ongezeko la gharama ya nishati ya kupikia kwa kutokuongeza bei huku tukihakikisha upatikanaji endelevu wa gesi safi na ya kuaminika,” alisema Deogratius.
Aliongeza kuwa kipaumbele cha kampuni hiyo kwa sasa ni kuhakikisha utulivu wa bei unaendelea ili kusaidia shughuli za kiuchumi, akibainisha kuwa gesi ya kupikia ni nishati muhimu kwa kaya nyingi pamoja na biashara ndogo ndogo nchini.
“Tunatambua kuwa gesi ya kupikia ni nishati muhimu kwa Watanzania wengi na lengo letu ni kuhakikisha kwamba inapatikana kwa bei nafuu huku tukidumisha usambazaji wa uhakika kote nchini,” alisisitiza.
Kwa upande wa usambazaji, kampuni hiyo imeeleza kuwa itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa gesi kupitia mtandao wake wa maghala 25 yaliyosambaa nchini, hatua inayolenga kufikisha huduma hiyo katika maeneo ya mijini na vijijini.
Deogratius alibainisha kuwa Tanzania ni nchi kubwa yenye mahitaji tofauti ya nishati, hivyo uwekezaji katika miundombinu ya usambazaji umezingatiwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa inaendelea kuunga mkono vipaumbele vya kitaifa vya nishati pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ilieleza kuwa matumizi ya gesi ya kupikia yanachangia kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza athari za moshi wa kuni na mkaa, sambamba na kulinda mazingira na kuchochea ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.

No comments:
Post a Comment