OWM-TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM– TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya, Mhe. Dkt. Jafari Seif, amesema kuwa hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya katika ngazi ya huduma za afya ya msingi nchini imeendelea kuimarika na kufikia kiwango cha kuridhisha ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akizungumza Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi kilichoongozwa na Waziri wa Afya, Mhe.Mohamed Mchengerwa, pamoja na wadau wa sekta ya afya, katika ofisi za Bohari ya Dawa (MSD), Mhe. Dkt. Seif amesema kuwa tathmini ya mwaka 2026 inaonesha hali ya upatikanaji wa dawa imefikia asilimia 89 katika hospitali, asilimia 88 katika vituo vya afya, na asilimia 88 katika zahanati.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi vilikusanya takribani Shilingi Bilioni 108, huku makusanyo hayo yakitarajiwa kuongezeka hadi kufikia Shilingi Bilioni 192 katika mwaka 2025/26.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuandaa na kusimamia miongozo, taratibu na miundo ya usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya. Lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa wafamasia kote nchini wanakuwa sehemu muhimu ya timu za menejimenti katika vituo hivyo, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.




No comments:
Post a Comment