Friday, April 03, 2026

TANZANIA NA URUSI ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Urusi zimeingia hatua mpya ya ushirikiano wa maendeleo baada ya kusaini hati ya makubaliano katika sekta ya uchukuzi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza miundombinu ya kisasa na kuongeza ufanisi wa usafirishaji nchini.

Makubaliano hayo yalisainiwa tarehe 03 Aprili 2026 jijini St. Petersburg, Urusi, pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Uchukuzi na Usafirishaji, yakihusisha Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania na Wizara ya Uchukuzi ya Shirikisho la Urusi.

Kwa upande wa Urusi, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Andrey Nikitin, alieleza kuwa nchi yake ipo tayari kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Russia–Africa 2023. Alibainisha kuwa ushirikiano huo utahusisha uwekezaji katika miundombinu ya kisasa, msaada wa kiufundi, pamoja na ushiriki katika miradi ya kimkakati yenye tija kwa pande zote mbili.

Naye Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, alisema makubaliano hayo yanaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kushirikiana na mataifa yenye uzoefu mkubwa na teknolojia ya hali ya juu.

Alifafanua kuwa kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika na ubadilishanaji wa utaalamu, mafunzo kwa wataalamu, pamoja na uhamishaji wa teknolojia utakaosaidia kuongeza ufanisi, ubora na ushindani wa miundombinu ya uchukuzi. Aidha, alisisitiza kuwa hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kujijengea nafasi imara kama kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

Kwa mtazamo mpana, makubaliano haya yanafungua ukurasa mpya wa fursa za uwekezaji, utafiti na ubunifu, huku yakichochea maendeleo ya rasilimali watu na kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.

#Tanzania #Urusi #Uchukuzi #Maendeleo #Uwekezaji #Diplomasia #Miundombinu #HabariZaLeo








No comments:

TANZANIA NA URUSI ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Urusi zimeingia hatua mpya ya ushirikiano wa maendeleo baada ya kus...