Thursday, April 16, 2026

Makamu wa Rais wa Zimbabwe akutana na CP Kaganda kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Kembo Mohadi, amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, ikiwa ni juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika tarehe 15 Aprili 2026 katika Ofisi Ndogo za Makamu wa Rais nchini Zimbabwe, yalilenga kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Zimbabwe na Tanzania.

Katika kikao hicho, Mhe. Mohadi alimshukuru Balozi Kaganda kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili kupitia kazi za ubalozi huku akieleza kuwa ushirikiano huo unaendelea kukua, ukichochewa na ziara za viongozi wa ngazi za juu na mawasiliano ya karibu ya kidiplomasia.

 Alisisitiza umuhimu wa kufanyika kwa Mkutano wa Tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC), ambao utatoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyopita pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza ushirikiano wa pande mbili.

Aidha akizungumzia masuala ya kiuchumi, Mhe. Mohadi alibainisha nafasi ya miundombinu ya usafiri katika kukuza biashara, akitolea mfano wa reli ya TAZARA, ambayo ina uwezo mkubwa wa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, hususan nafaka, kutoka Tanzania kwenda Zambia na baadae Zimbabwe.

Kwa upande wake, Balozi (CP) Kaganda amemshukuru Makamu wa Rais kwa muda wake na kujadili kwa kina masuala ya ushirikiano wa pande mbili ambapo alithibitisha utayari wa Serikali ya Tanzania kuandaa Mkutano wa Tisa wa Joint Permanent Commission (JPC) ambalo ni jukwaa rasmi la ushirikiano kati ya nchi mbili linalotumika kujadili, kupanga na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya maendeleo kiuchumi, na kidiplomasia huku lengo likiwa ni kuimarisha zaidi mahusiano hayo.

Amefafanua zaidi kuwa ubalozi unaendelea kuratibu mafunzo ya lugha ya Kiswahili nchini Zimbabwe, ambapo washiriki wengi ni maafisa wa  vyombo vya ulinzi na usalama, hatua inayochangia kukuza mawasiliano na ushirikiano wa kikanda.

No comments:

Makamu wa Rais wa Zimbabwe akutana na CP Kaganda kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Kembo Mohadi, amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo, Kamishna wa Po...