Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeibuka miongoni mwa taasisi tatu bora zilizotunukiwa tuzo ya ubora kwa ushiriki na mchango wake katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) linaloendelea jijini Mwanza.
Tuzo hiyo imetolewa baada ya TFS kuonyesha ubunifu na mshikamano mkubwa wa watumishi wake katika masuala ya monitoring and evaluation (MEL), pamoja na kuvutia washiriki kupitia huduma zake za elimu, ikiwemo apitherapy (utalii wa tiba kupitia mazao ya nyuki), elimu ya ufugaji nyuki na mbinu shirikishi za uhifadhi zilizowasilishwa kupitia mhusika maarufu wa TFS, Mr. Tree.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu, Prof. Dos Santos Silayo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali za Misitu, Dk. Zainabu S. Bungwa, alisema heshima hiyo inathibitisha dhamira ya TFS katika kuendeleza mifumo imara ya MEL nchini.
“Tunachukulia tuzo hii kama chachu ya kuongeza ari ya kuboresha zaidi mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili matokeo chanya yaendelee kuwafikia wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Dk. Bungwa.
Kongamano hilo, lililoanza Septemba 10, 2025, limewakutanisha wataalam wa ufuatiliaji na tathmini kutoka serikalini, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, likiwa na kaulimbiu ya mwaka huu:
“Kuimarisha Uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Jamii ili Kuwezesha Utendaji Bora na Maendeleo Endelevu.”
Uzinduzi rasmi ulifanywa Septemba 11, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ambapo alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kujenga utamaduni wa ufuatiliaji na tathmini ili kuongeza tija katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kongamano hilo linajumuisha mijadala, mafunzo na mawasilisho ya kitaalamu, na linatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment