Saturday, September 13, 2025

RUZUKU YA SH.MILIONI 250 YATOLEWA KWA WABUNIFU WA MATUMIZI BORA YA NISHATI










πŸ“Œ Kamishna wa Umeme asema Serikali itaendelea kuwawezesha vijana wabunifu katika teknolojia ya matumizi bora ya nishati

πŸ“Œ Wabunifu wa kike wapongezwa kujitokeza kwa wingi  matumizi bora ya nishati nchini

Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), imetoa ruzuku ya jumla ya Shilingi milioni 250 kwa wabunifu kumi waliofanya vizuri katika Mashindano ya Ubunifu na Ufanisi wa Matumizi Bora ya Nishati.

 Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga amekabidhi ruzuku hiyo akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba katika hafla iliyofanyika Septemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam. 

Hafla hiyo imewakutanisha wabunifu mbalimbali waliobobea katika nyanja ya ufanisi wa matumizi bora ya nishati katika maeneo matatu ambayo ni ubunifu kwenye vifaa vinavyotumia umeme kidogo, ubunifu kwenye miundombinu ya majengo yanayotumia umeme kidogo pamoja na ubunifu wa vifaa vinayoonesha matumizi ya umeme.

Mhandisi Luoga amefafanua kuwa wabunifu waliojitokeza kushindanishwa walikuwa wengi lakini baada ya uchambuzi wa kina kufanyika jumla ya washindi 10 walipatikana. 

Mha.Luoga ametanabaisha kuwa katika jitihada za kuhamasisha matumizi bora ya nishati nchini, serikali ilishazindua mikakati mbalimbali ya kitaifa  ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Matumizi Bora ya Nishati pamoja na Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano kuhusu Nishati Safi ya Kupikia.

Amesema lengo kuu la mikakati hiyo ni kuchochea matokeo chanya ya matumizi bora ya nishati kwa kuzingatia ubunifu unaofanywa na vijana katika kuendeleza teknolojia zinazochangia ustawi wa sekta ya nishati nchini.

Aidha, Mhandisi Luoga amebainisha kuwa kuongezeka kwa ubunifu wa vifaa vinavyotokana na matumizi bora ya nishati kutachangia mafanikio makubwa kwa taifa hasa katika kuimarisha upatikanaji wa nishati endelevu na rafiki kwa mazingira.

“Serikali itaendelea kuwafuatilia na kuwaunga mkono vijana wabunifu katika teknolojia ya matumizi bora ya nishati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)”amesema Mhandisi Luoga

Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati, imeishauri UNDP kusaidia katika kuweka mifumo ya matumizi bora ya nishati katika majengo ya Serikali yaliyo Mji wa Serikali wa Mtumba.

Hatua hiyo inalenga kuonesha mfano wa matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira katika taasisi za umma, sambamba na kuhamasisha matumizi bora ya nishati kwa ufanisi katika maeneo mengine ya Serikali.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), John Rutere amesisitiza umuhimu wa ubunifu wa ndani katika kuharakisha maendeleo ya jamii na kuimarisha mabadiliko ya nishati nchini Tanzania.

" Ninawapongeza wabunifu wa kike waliokuwa miongoni mwa washiriki wa mashindano ya ubunifu wa matumizi bora ya nishati kwani ushiriki wao unaonyesha ongezeko la ushirikishwaji wa wanawake katika sekta ya nishati na maendeleo ya taifa kwa ujumla” amesema Rutere

Ameeleza  kuwa hatua ya kuwawezesha na kuinua wabunifu, hususan wanawake, itaendelea kupewa kipaumbele ili kuhakikisha teknolojia bunifu za matumizi bora ya nishati zinaibuliwa  kwa kasi katika mataifa mbalimbali ya Afrika

No comments:

RUZUKU YA SH.MILIONI 250 YATOLEWA KWA WABUNIFU WA MATUMIZI BORA YA NISHATI

πŸ“Œ Kamishna wa Umeme asema Serikali itaendelea kuwawezesha vijana wabunifu katika teknolojia ya matumizi bora ya nishati πŸ“Œ Wabunifu wa kike...