Tuesday, September 23, 2025

MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA KAMATI YA KITUO CHA KUDHIBITI MAGONJWA AFRIKA (CDC)










New York, Marekani –
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha uthabiti wa Afrika katika kukabiliana na dharura za afya ya umma.

Akizungumza katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Dkt. Mpango alisema Tanzania imejipanga kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kutumia mbinu bunifu za ufadhili na kuunga mkono mipango ya kikanda inayolenga kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.

Makamu wa Rais alibainisha kuwa uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu na bidhaa nyingine muhimu za afya ni hatua ya lazima ili kuimarisha kujitegemea kwa Bara la Afrika. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye viwanda vya ndani, kuanzisha mamlaka za pamoja za udhibiti barani na kushirikiana katika uhawilishaji wa teknolojia kwa lengo la kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.

Aidha, Dkt. Mpango alikumbusha masomo yaliyopatikana kutokana na milipuko ya hivi karibuni ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Marburg, akisisitiza haja ya kuimarisha maandalizi na mifumo ya dharura ya kiafya. Alisema Tanzania inaendelea kuimarisha vitengo vya matibabu, kuandaa timu za dharura zinazoweza kupelekwa kwa haraka na kuwekeza katika miundombinu ya afya pamoja na rasilimali watu.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma ikiwemo ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, vifaa, udhibiti wa maambukizi na uratibu wa haraka katika kukabiliana na milipuko.

Makamu wa Rais pia alitoa wito wa mshikamano mkubwa kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda na Africa CDC kwa kuunda mbinu ya pamoja ya utafiti, sera na mipango ya kujenga uwezo, ili kuboresha uwezo wa pamoja wa kuzuia, kugundua na kushughulikia milipuko.

Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo: “Kuhakikisha Uhuru wa Afya Afrika: Uongozi wa Kisiasa kwa Ufadhili Endelevu wa Sekta ya Afya, Uzalishaji wa Ndani na Maandalizi Dhidi ya Milipuko ya Maradhi.”

Mazungumzo na Rais wa Ureno

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ureno, Mhe. Marcelo Rebelo de Sousa, pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Ureno katika sekta mbalimbali za maendeleo.

No comments:

MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA KAMATI YA KITUO CHA KUDHIBITI MAGONJWA AFRIKA (CDC)

New York, Marekani – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ...