Furaha na shangwe (chereko) zimetawala katika Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati wananchi walipofurika kununua majiko ya gesi na majiko banifu yanayouzwa kwa bei ya ruzuku katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Wananchi wengi waliokuwa wakipata huduma hiyo hawakuficha furaha yao, wakieleza kuwa hatua hiyo imewasaidia kupata majiko ya kisasa kwa gharama nafuu, hatua inayochochea mapinduzi ya nishati safi ya kupikia hasa vijijini.
“Kawaida majiko haya ni ghali, lakini kupitia REA tumeyapata kwa bei ya ruzuku. Hii ni neema kwa familia zetu na pia ni msaada mkubwa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni,” alisema mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo.
Katika maonesho hayo, REA imejipambanua kwa kuonyesha mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kulinda mazingira, kupunguza ukataji miti ovyo, na kuboresha afya za wananchi hasa akina mama wanaotumia muda mwingi jikoni.
Maonesho ya mwaka huu yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambaye alisisitiza dhamira ya Serikali kuendeleza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na kuongeza upatikanaji wa nishati safi na nafuu nchini.
REA, kupitia banda lake, limekuwa kivutio kikuu kwa wageni na wananchi waliohudhuria, huku wengi wakihamasika kununua majiko hayo na kujifunza mbinu mpya za matumizi yake.
Maonesho haya yanaendelea kutoa nafasi kwa wananchi na wadau mbalimbali kushuhudia teknolojia zinazobadilisha maisha ya Watanzania, huku REA ikionekana kuibua matumaini mapya ya kupikia kwa usalama, afya na gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment