Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kutekeleza mkakati kabambe wa kuboresha vituo vya utalii vilivyopo jijini Dodoma na Kanda ya Kati kwa ujumla, ili kuviinua kufikia hadhi ya kimataifa.
Mkakati huo unalenga kuimarisha miundombinu na huduma za kitalii katika maeneo ya Mkungunero, Hifadhi ya Swaga Swaga na Kituo cha Michoro ya Miambani cha Irangi kilichopo Kolo, wilayani Kondoa.
Akizungumza wakati wa ziara maalumu ya kitalii katika Kituo cha Michoro ya Miambani Kondoa Irangi, Kaimu Mkurugenzi wa Sehemu ya Uendelezaji Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dainess Kunzugala, alisema utekelezaji wa mkakati huo unafanyika kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau binafsi wa sekta ya utalii.
Alisema lengo ni kuhakikisha vituo hivyo vinatimiza vigezo vitano muhimu vya kimataifa ambavyo ni: miundombinu bora ya barabara, vifaa na huduma muhimu za utalii, hoteli za kisasa kuanzia nyota tatu, huduma kamili za kijamii na uwepo wa bidhaa pamoja na shughuli mbalimbali za kitalii zikiwemo burudani kwa familia na watoto.
*Ziara ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani*
Ziara hiyo, iliyopewa jina la “Nyama Choma Bata Pori”, iliratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na kampuni ya Epic Adventures, TTB na TFS ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani.
Mkurugenzi wa Epic Adventures, Joel Massai, alisema kampuni yake iliandaa ziara hiyo kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii nchini.
“Dodoma imebarikiwa vivutio vya kipekee vinavyohitaji jitihada za pamoja kati ya serikali na sekta binafsi ili kuviboresha na kuvitangaza,” alisema Massai.
*Wajibu wa TFS na TTB*
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TFS Kanda ya Kati, Mathew Kiondo, alisema Wakala unatekeleza mikakati mbalimbali kuboresha vivutio vya utalii vilivyopo katika kanda hiyo.
“Baadhi ya vivutio ikiwemo Mlima Hanang na michoro ya kale ya Kondoa Irangi vipo kwenye mapori ya akiba ambayo TFS inaendelea kuyaendeleza na kuyahifadhi ili kuchochea utalii wa mazingira,” alisema Kiondo.
Naye George Mwagane, Afisa Utalii Mwandamizi wa TTB Kanda ya Kati, alisema Bodi inatekeleza programu maalumu za kutangaza vivutio vya Dodoma kitaifa na kimataifa, huku miradi mikubwa kama Reli ya Umeme ya Mwendokasi (SGR) na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato ukiwa chachu ya kukuza utalii mkoani humo.
“Tunajipanga kuhakikisha dunia ya utalii inafika Dodoma,” alisema.
*Ongezeko la watalii Kondoa Irangi*
Meneja wa Kituo cha Michoro ya Miambani Kondoa Irangi, Zuberi Mabie, alisema uwekezaji wa serikali umechangia ongezeko kubwa la wageni wanaotembelea kituo hicho cha kihistoria.
Alisema idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 1,287 mwaka 2018 hadi 7,654 mwaka 2024, huku watalii wa kimataifa wakipanda kutoka 171 mwaka 2020 hadi 541 mwaka 2024.
“Sababu kuu za mafanikio haya ni pamoja na kuboreshwa kwa barabara, huduma bora za kijamii na matangazo ya kitaifa na kimataifa,” alisema Mabie.
*Maadhimisho ya mwaka huu*
Siku ya Utalii Duniani kwa mwaka huu iliadhimishwa Septemba 27 kwa kauli mbiu “Utalii na Maendeleo Endelevu.” Zaidi ya washiriki 40 kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, TFS, TTB na taasisi binafsi walihudhuria ziara ya siku mbili katika kituo hicho cha kihistoria kilichopo Kolo, Kondoa.
No comments:
Post a Comment