Addis Ababa, Ethiopia – 07 Septemba 2025 – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amewasili leo mjini Addis Ababa, akiwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Mkutano huu unaanza rasmi tarehe 08 hadi 10 Septemba 2025 na unalenga kuimarisha sauti ya Afrika katika mijadala ya kimataifa, kuongeza uhimilivu wa bara hili dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na kuendeleza ubunifu na juhudi za pamoja barani Afrika.
Utahudhuriwa na wawakilishi wa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti, pamoja na jamii asilia.
Aidha, Makamu wa Rais Dkt. Mpango anatarajiwa kushiriki katika mikutano ya kando yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na mataifa pamoja na mashirika mbalimbali yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania inasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuhakikisha Afrika inakabiliana vyema na changamoto za tabianchi na kuimarisha maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment