Monday, September 22, 2025

MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI TANAPA AFANYA ZIARA MKOANI TANGA








Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara, ameongoza Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa TANAPA katika ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Ujumbe huo uliwasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Tanga na kupokelewa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Bi. Catherine Mbena, ambaye pia ni Mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano wa TANAPA. Kutoka uwanjani, viongozi hao wameelekea wilayani Korogwe kwa ajili ya kushiriki shughuli za Ujirani Mwema, mpango unaolenga kuimarisha ushirikiano kati ya TANAPA na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.

Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa dhima ya TANAPA kuhakikisha uhifadhi unakwenda sambamba na maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi. Kupitia program za Ujirani Mwema, TANAPA hufadhili na kushirikiana na wananchi katika miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati, barabara na miradi mingine ya maendeleo, ikiwa ni njia ya kuongeza mshikikiano na uelewa juu ya faida za uhifadhi.

Akizungumza kabla ya kuelekea Korogwe, Mwenyekiti Jenerali Waitara alisisitiza dhamira ya TANAPA kuendeleza mshikamano na jamii ili uhifadhi uwe chachu ya maendeleo kwa taifa. Alisema, “Uhifadhi ni nguzo muhimu ya uchumi wa taifa, lakini nguzo hii inaimarika zaidi pale ambapo wananchi wanaona matunda yake moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.”

Aidha, ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya viongozi wa TANAPA kusikiliza maoni ya wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali wa uhifadhi, ili kuimarisha mikakati ya ushirikiano na kuhakikisha kwamba rasilimali za taifa zinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments:

MAJALIWA KUZINDUA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Septemba 22, 2025 amefungua maonesho ya nane ya teknolojia ya madini kwa mwaka 2025 ambayo yamefanyika kweny...