-AZINDUA KITUO CHA HUDUMA ZA UPANDIKIZAJI FIGO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali imedhamiria kuimarisha huduma za tiba za kitalii, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha na kuimarisha sekta ya afya nchini na kuchangia kwenye Pato la Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Ujenzi wa Kituo cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani pamoja na kuzindua Kituo cha Upandikizaji Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma. Amesema mchango wa Utalii wa Tiba kwenye Pato la Taifa kwa sasa unakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 166.5 ambapo idadi wa wagonjwa wanaokuja kutibiwa nchini imeongezeka kutoka 5,700 mwaka 2021 hadi 12,180 mwaka 2025.
Makamu wa Rais ametambua mchango wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa Utalii Tiba, unaotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Miundombinu, Vifaa tiba vyenye teknolojia ya kisasa na Wataalamu waliobobea katika maeneo mbalimbali. Amesema hatua hiyo inatoa fursa ya kuendelea kupanua huduma za Utalii Tiba zitakazowezesha wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kuja kwa wingi kutibiwa nchini.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ubia na Sekta Binafsi au Halmashauri ya Jiji kuangalia uwezekano wa kujenga jengo maalum kwa ajili ya huduma za malazi na nyinginezo kama chakula na fedha, kwa ndugu na wagonjwa wanaotoka nchi Jirani au mikoani, hususan pale wanaposubiri matibabu au kuruhusiwa kurejea makwao baada ya matibabu.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Wizara ya Afya, Madaktari na Wahudumu wote wa afya, kuhakikisha kuwa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na magonjwa inahusisha Shule, Vyuo, Taasisi za Kidini, NGOs, na Taasisi za Kijamii ili kuongeza jitihada katika kuwakinga Watanzania na magonjwa ya kuambukiza na hata yasiyoambukiza, ili kuepuka gharama kubwa za matibabu. Amewasisitiza kuwa wabunifu katika kutoa elimu kwa kutumia njia mbalimbali na hasa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na mifumo ya kidigitali ili kuwafikishia wananchi elimu hiyo muhimu.
Pia Makamu wa Rais ameilekeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao kuhakikisha mifumo ya matibabu katika Hospitali za kitaifa na zile maalum za kikanda inasomana ili kurahisisha mwendelezo wa matibabu.
Vilevile, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuweka utaratibu wa kuwasomesha na kuwaendeleza madaktari hadi kufikia ngazi ya ubingwa na ubobevu katika kutibu magonjwa ya saratani, upandikizaji wa figo na upandikizaji wa uboho.
Amesisitiza umuhimu wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuangalia uwezekano wa kuanzisha ushirikiano na wataalam wengine kutoka nje ya nchi kama vile Japan, Korea na mataifa mengine ili kuwajengea wataalamu wa nchini uwezo na kubadilishana uzoefu.
Amesema katika kuandaa Madaktari bingwa na bobezi itafaa mafunzo yao yatolewe sambamba na ya wataalam wengine husika, mfano mafunzo ya Daktari wa figo yaende pamoja na mafunzo ya wataalam wa damu, maabara, wauguzi, mionzi, na chakula na lishe.
Makamu wa Rais amewasihi Madaktari na Wahudumu wote wa afya katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali zote nchini kuzingatia kiapo cha maadili ya taaluma yao, kujituma na kutoa huduma zenye viwango na zinazomjali mgonjwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa katika sekta afya ikiwemo uboreshaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, wananchi kutoka mataifa mbalimbali Jirani wameendelea kupata matibabu katika Hospitali za hapa nchini.
Amesema Serikali ya Awamu wa Sita imeimarisha huduma za afya kuanzia katika zahanati hadi hospitali za kibingwa kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi kama ilivyoahidi kwa wananchi.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema katika kipindi cha miaka kumi ya hospitali hiyo, kumepatikana mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa huduma za ubingwa wa juukama vile matibabu ya magonjwa ya figo, upandikizaji wa uloto,matibabu ya magonjwa ya moyo, maabara maalum ya kuzibua mishipa ya damu, upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubongo, kubadilisha nyionga na magoti, matibabu ya homoni pamoja na matibabu ya watoto wachanga.
Ametaja mafanikio mengine kama vile, kuendesha mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni wenye uuwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku, uwepo wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi, kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa wa juu karibu na wananchi kupitia huduma mkoba na tembezi pamoja na kufanya tafiti za tiba kwa kushirikiana na taasisi zingine.
Katika hafla hiyo, Serikali imepokea rasmi mradi wa kimkakati wa Kituo cha Umahiri cha Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Magonjwa ya Damu kitakachojengwa hapa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma. Inatarajiwa kuwa mradi huu utakapokamilika utatatua changamoto ya matibabu ya upandikizaji uloto, katika hadhi ya ubingwa bobezi kwa kutoa huduma ambazo hazipatikani katika ukanda wa Afrika Mashariki.