📍Kibaha, Pwani – Machi 11, 2026
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) wametakiwa kuzingatia uadilifu, uwazi na weledi katika kuwasilisha na kushughulikia changamoto za watumishi wanaowawakilisha, ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa taasisi.
Wito huo umetolewa leo Machi 11, 2026 na Meneja wa Fedha na Mipango wa PBPA, Bw. Kedron Mbwilo, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa PBPA wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Pili cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Amesema Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu linalounganisha menejimenti na watumishi, hivyo wajumbe wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji mkubwa ili kuhakikisha masuala ya watumishi yanawasilishwa na kutatuliwa ipasavyo.
“Baraza la Wafanyakazi ni kiunganishi muhimu kati ya menejimenti na watumishi. Ni wajibu wa wajumbe kuwa waadilifu na kuwawakilisha watumishi wenzao kwa weledi mkubwa ili kuongeza tija na ufanisi katika taasisi,” amesisitiza Bw. Mbwilo.
Aidha, amewahimiza watumishi wa PBPA kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na kujituma ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo kwa upande wa sekta ya nishati inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na upatikanaji wa uhakika wa nishati ya mafuta, miundombinu imara ya mafuta pamoja na usimamizi bora wa rasilimali za petroli.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu wa PBPA, Bw. Matiko Sanawa, amewahimiza wajumbe wa baraza hilo kutumia kikao hicho kama fursa ya kujadili kwa uwazi maoni, mapendekezo na changamoto mbalimbali zitakazochangia kuimarisha uendeshaji wa taasisi.
Amefafanua kuwa kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi kinafanyika kwa mujibu wa matakwa ya kisheria na kwamba, pamoja na mambo mengine, kitajadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi na Bajeti kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Desemba 2026, pamoja na kuwasilishwa kwa rasimu ya Mpango Kazi wa PBPA kwa kipindi cha 2026/2027 hadi 2030/2031 na rasimu ya Bajeti ya PBPA kwa mwaka wa fedha 2026/2027.





No comments:
Post a Comment