Friday, August 22, 2025

Kaimu Mkurugenzi Mbarali Apokea Mkataba wa Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mafuta ya Alizeti








Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Bi. Gloria Komba, amepokea rasmi mkataba wa ujenzi wa jengo la kuchakata mafuta ya alizeti lililopo katika Kijiji cha Nyangulu, kutoka kwa Mratibu wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayanuai Tanzania (SLR), Dkt. Damas Mapunda.

Mradi wa SLR, unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, unalenga kurejesha mazingira yaliyoharibika, kuboresha mifumo ya ikolojia, na kuendeleza maisha bora ya jamii zinazozunguka maeneo yanayotekelezwa miradi hii. Kiwanda hiki cha kuchakata mafuta ya alizeti kitakuwa ni kipengele muhimu cha kuimarisha kilimo cha alizeti na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Nyangulu na maeneo jirani.

Makabidhiano ya mkataba yamefanyika leo, Agosti 22, 2025, wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Ofisi ya Makamu wa Rais, waliotembelea wilaya ya Mbarali ili kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Mradi wa SLR. Ziara hii imekuwa fursa ya kuthibitisha jinsi miradi ya kiasili na ya maendeleo ya kijamii inavyotekelezwa, ikiwapa wadau na viongozi fursa ya kuona matokeo ya uwekezaji na juhudi za kurejesha mazingira na kuimarisha ustawi wa jamii.

Mradi wa SLR unadhihirisha azma ya serikali ya kuendeleza miradi endelevu ya mazingira, huku ukiwa ni mfano wa ushirikiano kati ya serikali, jamii na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha maendeleo ya kiikolojia na kijamii yanapatikana kwa usawa.

MGODI WA DHAHABU WA GEITA KUWALIPA FIDIA WANANCHI KUPISHA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI




📍Geita.

Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi wa Mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, ili kupisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML). Hatua inayoleta suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 26. 

Akizungumza  Agosti 21, 2025 Mkoani Geita, Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikifuatilia kwa karibu changamoto za wananchi wa Geita na kutoa maelekezo mahsusi kuhakikisha zinatatuliwa kwa ufanisi.

 “Nawashukuru sana wananchi kwa uvumilivu wenu kwa zaidi ya miongo miwili. Leo hii tunatangaza suluhu ya mgogoro huu kwa sababu Serikali yenu inawajali na Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kutaka wananchi wapate haki zao bila usumbufu,” amesema Waziri Mavunde.

Mhe. Mavunde amebainisha kuwa GGML wameridhia kuanza mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa eneo la Nyakabale na Nyamalembo kwa mujibu wa utaratibu ili kupisha shughuli za mgodi. Amesema kuanzia kesho Agosti 22, 2005,  timu ya wataalamu wa Serikali itaanza kazi ya uthamini wa mali, na ndani ya siku 40 tathmini hiyo itakamilika ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao.

Aidha, Waziri ameeleza kuwa, mgogoro huo ulikuwa na hoja 13 za msingi ambazo zilihitaji kushughulikiwa, ambapo ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kutatua hoja 10 kati ya hizo na hatimaye leo kutatua hoja nyingine mbili.

Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, katika jitihada hizo, GGML imekubali kurekebisha mipaka yake ya leseni ya uchimbaji lna kuliachia eneo linalobaki kwa ajili ya wakazi wa maeneo hayo.

“Ninawapongeza viongozi wote mlioshiriki, hususan Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, na timu maalum iliyoundwa kushughulikia jambo hili kwa ufanisi mkubwa wamefanya kazi ya kupitia maoni ya wananchi na kuleta maoni ya wakazi hawa,  bila juhudi zao leo hii tusingefikia hatua hii” amesisitiza Mavunde. 

Pia, Waziri Mavunde ametumia nafasi hiyo kuwaonya na kuwakumbusha wananchi kuepuka tabia ya ‘tegesha’ kwani inaweza kukwamisha zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaostahili kupata haki zao kwa wakati na kuleta usumbufu kwa mwekezaji na wananchi. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kufuatilia kwa karibu mgogoro huo wa muda mrefu, na kumpongeza Waziri Mavunde kwa kusimamia utekelezaji kwa umakini.

“Wananchi wa Geita wamevumilia kwa muda mrefu. Tunawashukuru kwa ustahimilivu wao na tunahakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wote,” alisema Shigella.

Wananchi wanaotarajiwa kufanyiwa tathmini na kulipwa fidia ni wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo ndani ya Manispaa ya Geita.

Hatua hiyo ya Serikali inatazamwa kama historia muhimu ya kumaliza mgogoro wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 26 na uliokuwa unachangia sintofahamu kati ya wananchi na mwekezaji, na sasa inaleta matumaini ya maendeleo na mshikamano endelevu katika Mkoa wa Geita.

Thursday, August 21, 2025

Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha CCM chaguo la wagombea bunge






Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kilichofanyika leo, Agosti 21, 2025, Jijini Dodoma.

Kikao hiki kililenga kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa, ikiwa ni pamoja na:

  • Wagombea Ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

  • Wabunge wa Viti Maalum,

  • Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na

  • Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Viti Maalum.

Rais Samia Suluhu Hassan aliwashirikisha wajumbe wa kikao hiki mchakato wa kikatiba na uwajibikaji wa kuchagua wagombea wenye sifa bora, ili kuhakikisha uwakilishi unaoendana na matarajio ya wananchi na maendeleo ya taifa.

Wednesday, August 20, 2025

WAZIRI KOMBO AWASILI JIJINI YOKOHAMA (JAPAN) KUSHIRIKI MKUTANO WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA TICAD 9









Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili  jijini Yokohama, Japan kumwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD 9) ambao unafanyika kwa ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika na Japan kuanzia tarehe 20-22 Agosti 2025. 

Mheshimiwa Waziri Kombo amepokelewa na Mhe. Hideaki Harada , Balozi wa Zamani wa Japan nchini Namibia ambaye amekasimiwa jukumu la kumpokea Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania; Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda ambaye ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bi. Felista Rugambwa na Maafisa Wandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan. 

Mheshimiwa Waziri Kombo pamoja na kushiriki mkutano huo atafanya mazungumzo na Mhe. Takeshi Iwaya, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan; Bw. Ando Naoki, Makamu wa Rais wa JICA; viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi wa Japan; Wakuu wa Taasisi na kampuni za uwekezaji wa Japan kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji, biashara na utalii hapa nchini.

KASI NDOGO YA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA CHALINZE- DODOMA YAMKASIRISHA DKT. BITEKO









Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze  hadi Zuzu Dodoma na kueleza kutoridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo ambao  ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31 lakini kwa sasa  umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2024. 

Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika wakati Dkt. Biteko akikagua mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino mkoani Dodoma tarehe 20 Agosti 2025 ambapo Dkt. Biteko amemuagiza mkandarasi kampuni ya TBEA ya China kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa asilimia Saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.

Mwezi Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwani wakati mradi unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwemo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo. 

“ Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na asilimia 32 ya muda wote tuliokuwa tunahitaji  kutekeleza mradi huu, na tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31 lakini katika hali ya kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo halikubaliki.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi za kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki kwani  wananchi  hao wana haki na  lazima walipwe fidia.

Kutokana na hali hiyo, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)  kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.

Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa mkandarasi alishaagizwa asiutekeleze mradi huo kwa mazoea kutokana na umuhimu wake kwani kwa sasa  miundombinu inayosafirisha umeme kwenda  Dodoma kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) kupitia kituo cha  Chalinze  inabeba umeme kidogo kwa takriban megawati 240 tu ambayo ni sawa na mashine moja tu kati ya mashine 9 za JNHPP hivyo njia hiyo mpya ya umeme ya kV 400 inayojengwa ni muhimu.

Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu kwani katika Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongezka kila siku huku mkoa huo pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya Magharibi ikiwemo Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma ambayo inategemea utulivu wa umeme katika Mkoa wa huo na kwamba  Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo Mkandarasi ahakikishe kuwa anaupa umakini  mkubwa.

Kutokana na mradi huo kuwa nyuma katika utekelezaji,  Dkt. Biteko  amemuagiza Mkandarasi kuja na mpango mpya wa utekelezaji wa kazi ukiwemo wa kufidia muda uliopotezwa ambapo ametoa siku nne mpango wa fidia ya muda uwasilishwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.

Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza mkandarasi kuongeza nguvu kazi ya watu ili minara 917 ya umeme inayopaswa kujengwa kwenye mradi huo ijengwe kwani kwa sasa mkandarasi amechimba takriban  mashimo 100 tu kwa ajili ya usimikaji wa minara. Pia amemtaka Mhandisi mshauri wa mradi kuhakikisha anasimamia mradi huo kwa ufanisi na aeleze ukweli pale anapoona kuwa hauendi sawa.

Aidha amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutengeneza timu itakayoungana na TANESCO kuusimamia mradi huo na kila wiki taarifa itolewe kuwa umefikia wapi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wananchi kutozuia utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa hataki wananchi wafanyiwe dhuluma ambapo wasaidizi wake wanahakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema  mradi huo wa usafirishaji umeme wa kV 400 kunaenda kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha usambazaji umeme nchini.

Aidha, ameahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Dkt. Biteko ya kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha umeme huo utakaofikishwa Dodoma, kusambazwa pia kwenye maeneo mengine nchini.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange amesema Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unakusudia kusafirisha umeme wote unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (Megawati  2,115) na kuingiza kwenye gridi ya Taifa kisha  kuufikisha kwenye maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.

Amesema mkataba na mkandarasi kampuni ya TBEA ulisainiwa mwaka 2024 na mradi kuanza kutekelezwa mwezi Novemba 2024 ambapo mkandarasi ameshalipwa awamu ya kwanza ya malipo ambayo ni shilingi za kitanzania bilioni 107 na mhandisi mshauri ameshalipwa asilimia 15 ya malipo yake.

Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa  Nishati yatafanyiwa kazi ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mradi unakamilika mwezi Juni au kabla ya Juni 2026 kwa mujibu wa mkataba.

Aidha, Ameishukuru Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 513 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa na urefu wa kilometa 345 na kuhusisha minara ya umeme ipatayo 917 kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Zuzu mkoani Dodoma.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI AFANYA KIKAO KAZI NA WAKUU WA MKOA PWANI KUJADILI CHANGAMOTO ZA ARDHI






Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amefanya kikao kazi cha pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakary Kunenge, chenye lengo la kujadili na kutafuta suluhu za changamoto mbalimbali za ardhi zinazowakabili wananchi na sekta za umma na binafsi katika mkoa huo.

Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani leo, tarehe 20 Agosti 2025, na kilihudhuriwa na viongozi na wataalamu mbalimbali muhimu kwa masuala ya ardhi na usalama wa Mkoa. Miongoni mwa waliohudhuria ni:

  • Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa;

  • Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mheshimiwa Nickson Simon;

  • Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Shaibu Ndemanga;

  • Kamishna wa Ardhi, Bw. Mathew Nhonge;

  • Pamoja na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Katika kikao hicho, Waziri Ndejembi na Mkuu wa Mkoa walibainisha umuhimu wa kushirikiana kwa karibu kati ya Wizara na viongozi wa mikoa ili kuhakikisha changamoto za ardhi zinatatuliwa kwa wakati, ikiwemo masuala ya mipaka, usajili wa ardhi, migogoro ya umiliki, na changamoto zinazohusiana na uwekezaji. Aidha, walisisitiza kuwa lengo ni kuimarisha huduma za ardhi kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa kidijitali na kuhakikisha uwazi katika kila hatua ya usajili na utatuzi wa migogoro.

Kikao hiki ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za Serikali za kuimarisha usimamizi wa ardhi nchini, kutoa suluhu endelevu kwa changamoto za ardhi, na kuhakikisha kwamba ardhi inatumika kwa maslahi ya taifa na wananchi kwa usawa.

NAPLES ZOO YATOA MSAADA WA MAHEMA KUSAIDIA UHIFADHI WA FARU WEUPE NGORONGORO






Katika kuendeleza juhudi za kuimarisha uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, Taasisi ya Caribbean Naples Zoo kutoka Marekani imetoa msaada wa mahema kumi (10) kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Msaada huu una lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi wa faru weupe na wanyama wengine waliopo katika eneo la urithi wa dunia la Ngorongoro.

Mwakilishi wa Caribbean Naples Zoo Tanzania, Albert Mollel, ameashiria kuwa msaada wa vifaa hivi ni muendelezo wa ushirikiano wa kimataifa unaolenga kuimarisha ulinzi na uhifadhi endelevu wa wanyamapori, hususan aina adimu na zile zilizo hatarini kutoweka kama faru.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Bw. Abdul-Razaq Badru, amemshukuru Caribbean Naples Zoo kwa msaada huu muhimu. Pia alisisitiza kuwa vifaa hivyo vitawawezesha askari wa uhifadhi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi katika kulinda faru na wanyama wengine waliopo Hifadhi ya Ngorongoro

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA TISA WA TICAD 9 NCHINI JAPAN









Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zinazoshiriki katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 9), unaofanyika nchini Japan kuanzia tarehe 20 Agosti 2025.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi leo kwa pamoja na viongozi wakuu wa dunia akiwemo Mheshimiwa Shigeru Ishiba, Waziri Mkuu wa Japan; Mheshimiwa João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU); Mheshimiwa António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN); Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC); Bw. Haoliang Xu, Kaimu Mkurugenzi na Naibu Msimamizi wa UNDP; pamoja na Bw. Makhtar Diop, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kwa niaba ya Rais wa Benki ya Dunia.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Japan, Shigeru Ishiba, ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya Japan na Bara la Afrika kupitia maeneo makuu matatu: uchumi, jamii, na ulinzi na usalama.

Kwa kuzingatia mahusiano ya muda mrefu na ya heshima kati ya Japan na Afrika, Waziri Mkuu ameweka msisitizo mahsusi katika:

  • Kutafuta suluhu ya changamoto za madeni yasiyohimilika kwa baadhi ya nchi za Afrika;

  • Kuimarisha mtangamano na mshikamano wa Bara la Afrika;

  • Kuwezesha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) kwa kuongeza ushirikiano wa kikanda;

  • Kukuza sekta binafsi ya Afrika kupitia ushirikiano wa moja kwa moja na sekta binafsi ya Japan;

  • Kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu, hususan vijana na wanawake, kwa kupitia programu za mafunzo, ubunifu na startups;

  • Kuunga mkono juhudi za Afrika katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.

Kwa upande wake, Tanzania inaendelea kuthamini na kushirikiana na Japan katika kuimarisha maendeleo endelevu na kukuza ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii, kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Bara la Afrika kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi Mbarali Apokea Mkataba wa Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mafuta ya Alizeti

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali , Bi. Gloria Komba, amepokea rasmi mkataba wa ujenzi wa jengo la kuchakata mafuta ya al...