Tuesday, April 08, 2025

Dkt. Samia Aandika Historia Mpya Angola, Alihutubia Bunge la Taifa kwa Heshima ya Juu






 Luanda, Angola – Aprili 8, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka alama muhimu katika uwanja wa diplomasia ya kikanda baada ya kulihutubia rasmi Bunge la Jamhuri ya Angola jijini Luanda, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kiserikali nchini humo.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Dkt. Samia alisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa Afrika katika kuimarisha uchumi, kukuza biashara ya ndani ya bara, na kuhimiza amani na ushirikiano kati ya mataifa. Aligusia pia ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, hususan katika nyanja za elimu, afya, nishati, na uwekezaji.

“Ni wakati wetu sasa, kama mataifa ya Afrika, kusimama pamoja na kujenga mustakabali imara kwa vizazi vijavyo,” alieleza Mhe. Rais Samia mbele ya wabunge na viongozi waandamizi wa Serikali ya Angola.

Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuibua fursa mpya za kiuchumi na kijamii baina ya mataifa haya mawili marafiki.

WAZIRI NA NAIBU WAZIRI WA ARDHI WASHIRIKI KIKAO CHA KWANZA CHA MKUTANO WA 19 WA BUNGE LA 12 KWA AJILI YA KUJADILI BAJETI YA SERIKALI 2025/2026







Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi (MB), leo tarehe 8 Aprili 2025, ameshiriki kikao cha kwanza cha Mkutano wa 19 wa Bunge la 12, kilichofanyika katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma. Mkutano huo ni maalum kwa ajili ya kuanza rasmi mchakato wa kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Pamoja naye, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Geofrey Pinda (MB), naye alihudhuria kikao hicho cha awali, akionesha mshikamano na ushiriki wa viongozi wote wa Wizara katika kujadili mipango ya maendeleo inayolenga kuboresha ustawi wa Watanzania kupitia sekta ya ardhi, nyumba, na maendeleo ya makazi.

Kupitia kikao hicho, Bunge linatarajiwa kupokea, kuchambua, na kujadili mapendekezo ya bajeti kutoka kwa wizara mbalimbali, huku likijielekeza katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinasimamiwa ipasavyo kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu na jumuishi.

Kwa upande wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, bajeti ya mwaka 2025/2026 inatarajiwa kuelekeza nguvu zaidi katika kuboresha upatikanaji wa ardhi iliyopangwa na kupimwa, kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba bora na nafuu kwa Watanzania, pamoja na kuendeleza usimamizi madhubuti wa rasilimali za ardhi ili kuchochea uwekezaji na maendeleo ya miji.

Ushiriki wa viongozi hao wakuu wa wizara katika kikao hiki muhimu ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa vitendo kupitia mijadala ya kina na maamuzi ya kibajeti yenye tija kwa taifa.

WALIOSHINDWA KUREJESHA MAWASILIANO SOMANGA KUCHUKULIWA HATUA: ULEGA



Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesisitiza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wataalam kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) 

waliouhusika na uzembe wa kushindwa kurejesha kwa wakati mawasiliano ya barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi eneo la Somanga Mtama Mkoani Lindi

Ulega ameeleza hayo Mkoani Lindi wakati alipofika na kukagua kazi za urejeshaji wa mawasiliano hayo yaliyokatika tarehe 06 Aprili, 2025 na kutoridhishwa na kasi ya urejeshaji wa mawasiliano hayo na kuelekeza wataalam kutoka kwa TANROADS kutoondoka eneo hilo hadi mawasiliano hayo yatakaporejea.

“Nimekagua na nimeona namna kazi inavyoendelea, mimi kama Kiongozi nimeona kuna jambo ambalo bado halijafanyika kisawasawa, uko uzembe uliofanyika, nitachukua hatua kali ili siku zingine yatakapotea mambo ya dharura kama haya yachukuliwe kidharura”, amesema Ulega.

Ulega ametoa salamu za pole kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na Dar es Salaam waliokumbwa na kadhia hiyo na kuwahakikishia kuwa timu ya wataalam iliyopo itafanya kazi haraka iwezekanavyo ili kuruhusu wananchi waliokwama kuendelea na safari zao. 

Halidhalika, ameipongeza timu ya wataalam ya TANROADS Mkoa wa Lindi kwa kuchukua jitihada za dharura mara baada ya tukio hilo kutokea na kusisitiza kuongezwa kwa idadi ya malori ya mawe hadi kufika magari 100 ili yasaidie kwa haraka urejeshaji wa barabara katika eneo hilo.

Akizungumza na wananchi wa Somanga, Ulega ameeleza kuwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha zaidi ya Shilingi Bilioni 130 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja yaliyokatika katika Mkoa wa Lindi na kubainisha kuwa hatua za ujenzi wa madaraja matano zinaendelea na yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ameongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo na katika mwaka mpya wa fedha 2025/2026 itakarabati na kuziba mashimo katika maeneo korofi ya Marendego, Somanga, Njia Nne, Matandu, Ikwriri - Nyamwage - Chumbi ili kurahisisha huduma za usafiri wa abiria na mizigo.

Vilevile, Serikali itaanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara kwa njia nne kuanzia Kongowe - Mbagala Rangi tatu ambapo tayari Mkandarasi ameshapatikana na pia ujenzi wa barabara kuanzia Kongowe hadi Mkuranga itajengwa kwa njia nne ili kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa.

Sunday, April 06, 2025

WAZIRI MKUU AWATAKA MABALOZI KUISHI FALSAFA ZA RAIS DKT. SAMIA




WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka mabalozi kuiishi falsafa ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha mahusiano na kukuza diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, kilimo, biashara pamoja na kupata masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Aprili 6, 2025) alipokutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Balozi Hamad Khamis Hamad Balozi wa Tanzania nchini Msumbuji na Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi, Balozi wa Tanzania nchini Sweden.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ina mategemeo makubwa na mabalozi hao, hivyo wanapaswa kwenda kuendeleza mahusiano mazuri ya muda mrefu yaliyopo baina ya Tanzania na mataifa hayo.

Waziri Mkuu amesema pamoja na mambo mengine mabalozi hao wanatakiwa wahakikishe wanasimamia vizuri matumizi ya fedha katika ofisi zao pamoja na kuanzisha au kuendeleza madarasa ya kufundisha lugha ya kiswahili.

MRADI WA KUFUA UMEME WA JNHPP WAKAMILIKA RASMI: DKT BITEKO

 









-Asema ni ndoto ya watanzania,awataka wategemee umeme wa uhakika

-Asisitiza kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia wananchi umeme

-Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri kuuzindua rasmi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kutegemea kupata umeme wa uhakika baada ya Mradi wa kufua umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania kukamilika rasmi.

Waziri Biteko ameyasema hayo leo April 5, 2025 baada ya kutembelea Mradi huo akiwa ameambatana na Mawaziri ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mha. Hamadi Masauni.

Amesema hivi sasa mitambo yote tisa inafanya kazi ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa Mradi huo kumechangiwa na maono ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye aliupokea Mradi ukiwa katika asilimia 33 ya utekelezaji wake na ndani ya kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake ameweza kuukamilisha Mradi.

‘’Tumekuja leo tukiwa na furaha kubwa kwamba mitambo yote tisa imekamilika inazalisha umeme na nina furahi kuwajulisha Watanzania kuwa ile ndoto ya kuwa na umeme kutoka kwenye chanzo hiki kikubwa barani Afrika imekamilika, kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia watanzania umeme’’ Alisisitiza Dkt Biteko.

Dkt. Biteko amesema kutokana na nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kukamilisha mazungumzo na nchi ya Zambia kwa ajili ya kuwauzia umeme na tayari njia ya umeme ya kuunganisha nchi hizo mbili inajengwa.

‘’Kile ambacho tumekua tukikiongea miaka mingi kwamba Tanzania itakuwa na uwezo wa kuuza umeme nje ya nchi sasa imetimia katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita baada ya msukumo mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tuna mshukuru sana Mheshimiwa Rais’’

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe.Profesa Kitila Mkumbo amesema kukamilika kwa Mradi huu ni ukombozi wa kiuchumi huku Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamadi Masaun amesema Tanzania imeingia katika historia barani Afrika ambapo amesema kazi kubwa iliyobaki ni kutunza vyanzo vya maji ili kuulinda Mradi.

Katika hatua nyingine Mhe Dkt Doto Biiteko amelishukuru Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa utekelezaji wa Mradi kwa kiwango cha kimataifa na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga kwa usimamizi na jitihada zake katika kusimamia miradi mbalimbali ya umeme.

Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere umegharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 6.5 ambapo mpaka sasa serikali imeshalipa zaidi ya asilimia 99.5.

Friday, April 04, 2025

MAKAMU WA RAIS MHE. DKT. PHILIP MPANGO AONGOZA KIKAO CHA 15 CHA KAMATI YA PAMOJA YA MASUALA YA MUUNGANO




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameongoza Kikao cha 15 cha Kamati ya Pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) cha kushughulikia masuala ya Muungano. Kikao hiki kimefanyika leo, tarehe 04 Aprili 2025, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umejikita katika kujadili na kutafuta suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazohusu Muungano, huku ukilenga kuimarisha mshikamano, ushirikiano, na maendeleo kati ya pande mbili za Muungano. Viongozi wa pande zote mbili wameonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha masuala yanayohusu Muungano yanashughulikiwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya Watanzania wote.

MTAA WA MAKANGIRA DAR ES SALAAM KUPANGWA NA KUENDELEZWA UPYA











Serikali imeanzisha Programu ya kuendeleza miji iliyochakaa kwa kuboresha makazi pasipo kuwahamisha mwananchi hata mmoja kutoka katika eneo analomiliki.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.  Deogratius Ndejembi Aprili 04, 2025 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Makangira, Kata ya Msasani wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam wakati akitambulisha program hiyo.

“Katika program hii, hakuna mwananchi hata mmoja atahamishwa, tumedhamiria kuboresha makazi yenu pasipo kuhamishwa kwa mwananchi hata mmoja kutoka katika eneo analoishi isipokuwa kwa wananchi wachache ambao utekelezaji wa mradi utakapoanza, Serikali itawapangishia nyumba wakati mradi ukiendelea kutekelezwa na baada ya kukamilika kwa mradi mtarejea katika maeneo yenu” amesema Waziri Ndejembi. 

Waziri Ndejembi amesema kwa kuzingatia matakwa Sera ya Taifa ya mwaka 1995 Toleo la mwaka 2023 ambayo imezinduliwa hivi karibuni na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Programu hiyo maalum ya uendelezaji upya maeneo chakavu katika miji ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa huduma za msingi, miundombinu, makazi duni au chakavu, ukosefu wa mifumo ya maji taka na uwepo wa changamoto ya taka ngumu zinapelekea uchafuzi wa mazingira. 

Wizara imetambua jumla ya maeneo 111 katika mikoa 24 ambapo kwa kuanzia Programu hiyo itatekelezwa katika majiji ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Mwanza Mbeya na Tanga.

Waziri Ndejembi amesema program hiyo ina faida lukuki ikiwemo upatikanaji wa ardhi iliyopangwa kwa matumizi mbalimbali ambayo ni kichocheo cha ongezeko la shughuli za kiuchumi na kijamii, upatikanaji wa nyumba hususani za makazi na biashara na kutatua changamoto ya makazi duni katika maeneo ya miji nchini, kuboresha madhari ya miji yetu na kuongeza usalama wa milki za wananchi katika maeneo husika kwa kupatiwa hati za sehemu ya jengo na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kugeuza ardhi mfu kuwa na thamani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Saad Mtambule amesema program hiyo itakuwa suluhisho la changamoto ya mafuriko, magonjwa ya mlipuko, migogoro ya ardhi na itasaidia kuongeza thamani ya ardhi katika eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya maji na barabara hatua itakayoboresha makazi ya wananchi wa eneo la Makangira jijini Dar es salaam.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Songoro Mnyonge amesema ujio wa program hiyo umekuja muda mwafaka ambapo manispaa hiyo mwaka 2013 ilipitisha Mpango wa Kuboresha  Makazi ili kupata nyumba bora za wananchi wa manispaa hiyo.

BALOZI DKT. NCHIMBI AZUNGUMZA NA WANANCHI WA NAMTUMBO










Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na umati mkubwa wa wananchi Namtumbo, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Namtumbo, leo Alhamis tarehe 3 Aprili 2025.

Katika mkutano huo, viongozi wa vyama vya ACT Wazalendo na Chadema, wakiwaongoza wanachama wao, waliamua kurejesha kadi na vifaa vingine vya vyama hivyo, kisha wakajiunga CCM.

Viongozi hao, akiwemo Ndugu Alifa Jafa, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Songea, Ndugu Mohamed Said Ndauka, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ntungwe na Azarius Lucas Ngonyani, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembeni, walieleza jinsi ambavyo uongozi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuteuliwa kwa Balozi Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Urais, kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025, umewavutia kuhamia CCM.

Dkt. Samia Aandika Historia Mpya Angola, Alihutubia Bunge la Taifa kwa Heshima ya Juu

  Luanda, Angola – Aprili 8, 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka alama muhimu katika ...