DKT.MWAKYEMBE AMEWAPONGEZA WAJASIRIAMALI WA TANZANIA KWA KUSHIRIKI TAMASHA LA JAMAFEST KAMPALA, UGANDA
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
(kushoto) akiangalia ngoma ya kiutamaduni iliyokuwa ikipigwa na Kikundi
cha Sanaa na Utamaduni Tanzania (TaSUBA) katika banda lao wakati wa
Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika
mjini Kampala, Uganda 13 Septemba, 2017.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
(kushoto) akimsikiliza mjasiriamali wa Tanzania kuhusu baadhi ya bidhaa
zilizopo katika banda lao wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika
Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13 Septemba,
2017.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
(kulia) akipokea zawadi ya shati toka kwa mjasiriamali wa Tanzania mara
alipotembelea banda lao wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika
Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13 Septemba,
2017.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
(mwenye tai nyekundu) akiangalia moja ya ubunifu wa picha iliyochongwa
na mjasiriamali wa Tanzania wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa
Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika mjini Kampala, Uganda 13
Septemba, 2017.PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
amewapongeza Wajasiriamali wa Tanzania kwa ushiriki wao katika Tamasha
la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST.
Dkt.
Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo mjini Kampala nchini Uganda katika
viwanja vya Mashujaa Kololo alipotembelea kujionea namna tamasha hilo
lilivyopokelewa na wadau wake walioiwakilisha Tanzania wakiwemo
wajasiriamali toka vikundi mbalimbali, vikundi vya ngoma, vikundi vya
sanaa ya maigizo pamoja na baadhi ya wasanii.
Katika
tamasha hilo, Dkt. Mwakyembe pia alipata fursa ya kutembelea baadhi ya
mabanda ya wajasiriamali hao pamoja na kuongea nao huku akijionea bidhaa
mbalimbali zinazouzwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
jambo ambalo limemfurahisha sana hususani kwa upande wa watu kutoka
Tanzania kwakuwa wamejaza mabanda yao kwa bidhaa kadha wa kadha.
“Tamasha
hili linaonyesha utajiri mkubwa wa sanaa, utamaduni pamoja na bidhaa
tulizonazo kama nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na hapa
tumekutana kwasababu tunabadilishana mawazo na kuonyeshana bidhaa
mbalimbali za nchi zetu”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha,
katika ziara hiyo, Dkt. Mwakyembe amewatoa wasiwasi wajasiriamali hao
kuhusu suala la upatikanaji wa masoko huku akiwaahidi kuwatafutia fursa
ya kuwapeleka wajasiriamali hao pamoja na bidhaa zao Bungeni mjini
Dodoma ili ziweze kupata soko kwa urahisi kupitia wabunge.
“Niwatoe
wasiwasi wajasiriamali wote wa Tanzania mliohudhuria hapa,
nitahakikisha kuwa pindi tunaporudi nyumbani nitatafuta wasaa wa
kulishawishi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili nyie mpate
nafasi ya kuleta bidhaa zenu katika viwanja vya Bunge ili basi Wabunge
wapate kujua haswa vitu vizuri mlivyonavyo nah ii itawasaidia kuviuza
kwa urahisi zaidi na kujipatia vipato vyenu”, aliongeza Dkt. Mwakyembe.
Sambamba
na hilo, Dkt, Mwakyembe amewahakikishia wajasiriamali hao kuhusu suala
la kujitangaza kupitia vyombo vya habari akisema kwamba, atajitahidi
kutoa ushawishi kwa vyombo vya habari nchini ili viweze kuwapatia muda
wa kuwatangaza wajasiriamali hao ili wapate kujulikana ikiwemo shughuli
wazifanyazo.
“Nitahakikisha
kuwa siku mnapopewa nafasi ya kuja viwanja vya Bunge basi mnapata muda
wa kutosha katika vyombo vya habari ili mpate kujulikana, hivyo kila
mmoja wenu naamini atapewa nafasi ya kufanya mahojiano kwa kujieleza
shughuli azifanyazo na mahali anapopatikana na hii itawasaidia kupata
masoko zaidi toka kwa watu mbalimbali”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa
upande wao wajasiriamali hao wameshukuru Waziri Mwakyembe kwa juhudi
alizowafanyia hususani za kuhakikisha kwamba wanahudhuria kwa kiwango
kikubwa katika tamasha hilo, lakini pia ahadi aliyowapa ya kuwapeleka
Bungeni ili wakatangaze bidhaa zao na kuwatangaza katika vyombo vya
habari nchini.
Tamasha
la JAMAFEST lilianzishwa mwaka 2013 nchini Rwanda na baadhi ya Viongozi
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa mwaka huu tamasha hilo
linafanyika mjini Kampala nchini Uganda ambapo pia tamasha hili
linatarajiwa kufanyika tena katika moja ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2019.
Comments