PCCB: Vitendo vya Rushwa Vyazidi Kupungua Nchini

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wajumbe wa Kamati za kudhibiti uadilifu kuhusu utekekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa, awamu ya tatu (2017-20120)  jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bibi. Theresia Mmbando na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Bw. Edward Mpogolo.
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Bibi. Theresia Mmbando akielezea jambo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wajumbe wa Kamati za kudhibiti uadilifu kuhusu utekekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa, awamu ya tatu (2017-20120)  jijini Dar es Salaam.
 Mratibu wa Kitengo cha Utawala Bora kutoka Ofisi ya Rais Bi. Christina Maganga akitoa neno la utangulizi kuhusu mkakati wa taifa dhidi ya rushwa awamu ya tatu wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wajumbe wa kamati za kudhibiti uadilifu kuhusu utekekelezaji wa mkakati huo  jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudhibiti uadilifu kutoka mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia wakifuatila mada wakati wa kikao kazi cha wajumbe wa kamati hizo kuhusu utekekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa, awamu ya tatu (2017-20120)  jijini Dar es Salaam.
 Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo akisikiliza kwa makini maelezo kuhusu mkakati wa taifa dhidi ya rushwa toka kwa Mratibu wa Kitengo cha Utawala Bora Ofisi ya Rais, Bi. Christina Maganga (hayupo pichani) wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha wajumbe wa Kamati za kudhibiti uadilifu jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bibi. Theresia Mmbando na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Bw. Edward Mpogolo.
Mkuu wa Takukuru Kanda Maalum ya Dar es Salaam Juventus M. Baitu akiwasilisha mada kuhusu hali ya rushwa katika mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kikao kazi cha wajumbe wa Kamati za kudhibiti uadilifu kuhusu utekekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa, awamu ya tatu (2017-20120).
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo  akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha wajumbe wa Kamati za kudhibiti uadilifu kuhusu utekekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa, awamu ya tatu (2017-20120)  jijini Dar es Salaam.
Picha zote na: Frank Shija- MAELEZO.

Na. Paschal Dotto- MAELEZO.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya  uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya rushwa katika ofisi za Serikali, taasisi na mashirika ya umma na kuweka usawa katika  upatikanaji wa huduma kwa jamii.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam  na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John  Mbungo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kuhusu rushwa katika taasisi na mashirika ya umma kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
 Brigedia Jenerali Mbungo alisema kuwa lazima watumishi wajifunze kuwa waadilifu, kwa hiyo kile watakachokipata kutoka katika mkutano huo kikafanye kazi kuleta haki kwa wananchi wakati wa kupata huduma katika ofisi zao ili kuendana na sera ya Awamu ya Tano ya kutokuvumilia vitendo vya rushwa nchini.

“Tumieni fursa katika kikao hiki ili kuweza kupata elimu itakayosaidia wananchi kuelimika juu ya vitendo vya rushwa na kupata haki zao za msingi wanapopata huduma katika ofisi zenu”,alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Kikao kazi hiki ni cha kwanza ambacho kinafuatia mkakati wa awamu wa tatu  utakaokuwa wa miaka mitano kuanzia  Julai, 2017 unaolenga kuanzia ngazi za vijiji, wilaya, mkoa, mpaka taifa ili kudhibiti uadilifu, nidhamu na utendaji kazi wenye kuzingatia haki katika ofisi mbalimbali nchini.

Aidha Brigedia Mbungo alisema kuwa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali, hali ya rushwa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa kwani malalamiko yamepungua katika ofisi, taasisi na mashirika ya umma.

“Hali ya rushwa sasa hivi imepungua kwa sababu Serikali kwa kutumia juhudi  mbalimbali imedhibiti hali hii, Tanzania ina viwango vya chini sana vya rushwa ikilinganishwa na nchi nyingine za maziwa makuu kwa hiyo naweza kusema kiwango kimepungua sana hususani kwa Jiji la Dar es Salaam ambapo vitendo hivi vilishamiri sana, hivyo katika awamu hii ya tatu ya mkakati huu tunatarajia viwango vitashuka zaidi”, alisisitiza Brigedia Jenerali Mbungo.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Bi.Theresia Mmbando alisema kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam hali ya vitendo vya rushwa imepungua kwa kiasi kikubwa na sasa wananchi wanapata huduma pasipo kuwa na dalili zozote za rushwa.

“Hali ya rushwa katika mkoa wetu wa Dar es Salaam inapungua siku hadi siku kwa kuwa watu wanaendelea kupata elimu ya haki zao za msingi na kuhudumiwa pasipo kutoa rushwa, wala kuwepo dalili za rushwa”, alisema Bi. Mbando.

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU,  kanda maalum ya Dar es Salaam Bw.Juventus Baitu ameeleza kuwa wamefanikiwa kuweka sawa  mkakati huo kwa kutoa elimu kwa wananchi na kwa sasa kumekuwa na mwamko wa kuripoti matukio ya rushwa katika ofisi yake.

Aliongeza kusema kuwa katika kitengo cha Dawati la Uchunguzi wamepokea malalamiko yapatayo 665 kwa mkoa wa Dar es Salaam huku kitengo hicho kikifungua majalada ya kesi 40 kwa Mwendesha Mashtaka (DPP) na kusikilizwa kesi 26 ambapo taasisi  hiyo ilifanikiwa kushinda kesi 14 na kuokoa kiasi cha pesa kisichopungua shilingi milioni 791,443,984 katika kesi mbalimbali za rushwa.

Aidha TAKUKURU kupitia dawati la elimu ya rushwa imeweza kufungua vilabu 94 vipya katika shule mbalimbali mkoani Dar es Salaam, kuendesha semina 91 kwa watumishi wa taasisi na mashirika ya umma pamoja na maonesho 12 yanayohusu vitendo vya rushwa ikiwemo kuwahabarisha wananchi kupitia vipindi vya televisheni 14 kuanzia mwaka 2016 pamoja na kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari kwa kutoa vitini 19 kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.

“Tumeweza kutoa elimu kupitia matamasha mbalimbali zaidi ya 16 katika taasisi na mashirika ya umma ambapo matamasha 7 yalikuwa na lengo la kutoa mazimio kwa taasisi na mashirika ya umma kuhusu kwa vitendo vya rushwa”,alisisitiza Bw.Baitu.Mkakati huo kwa awamu ya tatu ulizinduliwa rasmi, Desemba 10, 2016 wakati wa maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu duniani  na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo utekelezaji wake ulianza tarehe 1, Julai, 2017.

Comments