JAFO AWATAKA WATENDAJI MANYONI KUSIMAMIA MIRADI IPASAVYO

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu wakikagua chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua magodoro katika wodi ya wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua chumba cha dawa katika Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua mradi wa maji Kintinku wilayani Manyoni.



NAIBU waziri wa Nchi ofisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo amefanya ziara katika kituo cha Afya cha Kitinku kilichopo wilayani Manyoni mkoani Singida na kueleza dhamira ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kuboresha na kujenga miundombinu.

Akizungumza katika ziara hiyo JAFO amesema uboreshaji wa kituo hicho unatarajia kugharimu kiasi cha Sh.Milioni 500 na kwamba tayari serikali imeshaingiza kiasi hicho cha fedha.

Jafo amesema uboreshaji huo utajumuisha ujenzi wa chumba cha upasuaji,chumba cha kuhifadhia maiti,wodi ya kisasa ya akina mama na maabara na kuwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha hadi desemba 30, mwaka huu ujenzi huo uwe umekamilika.

“Awamu ya kwanza zimeingizwa shilingi milioni 500 kwa ajili ya miundombinu na baada ya ujenzi kukamilika serikali itaweka vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 220,nataka ujenzi huu uende kwa kasi atakayeleta masihara atajuta,”alisema Jafo.

Amewataka watendaji kutimiza wajibu kwa kusimamia malighafi zitumike vizuri na mafundi wajenge majengo kwa ubora na kusisitiza kuwa mafundi wa kujenga majengo hayo watatoka wilayani humo.

Naibu Waziri Jafo amemtaka Mganga Mkuu wa wilaya Dk.Nelson Bukuna kuhakikisha anawajibika ipasavyo kwa kutembelea mara kwa mara kwenye zahanati na vituo vya afya badala ya kusubiri hadi kiongozi afike.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Miraji Mtaturu na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Charles Fussi wameahidi kuhakikisha wanatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na serikali na ujenzi wake utafanyika kwa viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, Jafo ametembelea mradi wa maji wa Kitinku na kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Manyoni Charles Fussi kuhakikisha anasimamia timu yake ili azma ya serikali ya kuhakikisha wanamtua ndoo mama ndoo ya maji kichani inafanikiwa kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)inavyosema.Jafo amesisitiza uaminifu na kufanya kazi kwa kasi ili wananchi wapate huduma ya maji wanayotarajia.

“Katika utekelazaji wa miradi hii wakandarasi wengi sio waaminifu,Mkurugenzi hii ni sehemu ya kupima performance yako,usilale hakikisha watu wanapata maji,”amesema Jafo.Kwa upande wake mhandisi wa maji wilaya Gasto Mbondo amesema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 9.9 na utahudumia wananchi elfu 45,417 wa vijiji 11.

“Mradi huu unatekelezwa kwa awamu tano,na changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni upungufu wa wataalamu wa maji,ukosefu wa gari la kubebea mizigo ya maji na ukosefu wa fedha za kuendesha ofisi,”amesema Mbondo.Naye kaimu Mkuu wa wilaya hiyo, Miraji Mtaturu amepongeza na kumhakikishia Naibu waziri huyo kuwa atasimamia utekelezaji wa mradi huo na kwamba wilaya yake imeweka utaratibu wa kupokea taarifa kwa kina kuhusu miradi ya maji kila mwezi.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Manyoni Mashariki Daniel Mtuka ameishukuru serikali kwa jitihada zake za kutatua kero ya maji katika jimbo hilo na kwamba kwa muda mrefu wananchi wake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo.

Comments