Saturday, February 21, 2026
Compact Energies: Nishati ya Jua Ni Chachu ya Mageuzi ya Uchumi Tanzania
AKWILAPO AONGOZA MAWAZIRI KIKAO CHA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MASHAMBA YA UWEKEZAJI MUHEZA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Pius Chaya (Kulia) akisisitiza jambo wakati kikao cha kujadili utatuzi wa migogoro ya mashamba ya uwekezaji kwenye wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga. Katikati ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Leonard Akwilapo na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo (wa pili kulia) akizungumza wakati wa kikao cha kujadili utatuzi wa migogoro ya mashamba ya uwekezaji katika wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga. Wa pili kushoto ni Waziri wa TAMISEMI Prof Riziki Shemdoe na kulia ni Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji Dkt. Pius Chaya na Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Muheza Ayubu Sebabili.
Na Munir Shemweta, WANMM MUHEZA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo amewaongoza Mawaziri wenzake wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Ofisi ya Raisi Mipango na Uwekezaji katika kikao cha kujadili utatuzi wa migogoro ya mashamba ya uwekezaji katika wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.Kikao hicho kimefanyika tarehe 18 Februari 2026 katika ofisi ya Mkuu wa wilaya Muheza mkoa wa Tanga ikiwa ni utekelezaji wa masuala yaliyojitokeza wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mawaziri hao ni Prof. Riziki Shemdoe, Waziri wa TAMISEMI na Dkt. Pius Chaya, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji ambao kupitia kikao hicho, kilichohusisha pia wataalamu, viongozi hao walipata fursa ya kuwahoji wananchi walioguswa na migogoro hiyo ya mashamba ya uwekezaji ambayo yaliyofutiwa umiliki mwaka 2016.
Mashamba hayo ni Azimio/ Kilapula Geiglitz, Bwembwera, Kibaranga, Kihuhwi, Lewa pamoja na Saguras yaliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.
Baadhi ya wananchi walioguswa na mgogoro wa mashamba ya uwekezaji katika halmashauri ya Muheza mkoa wa Tanga wakielezea umiliki wao wa maeneo kwenye mashamba hayo mbele ya mawaziri wakati wa kikao cha kujadili utatuzi wa migogoro ya mashamba ya uwekezaji tarehe 18 Februari 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
DAS KAHAMA AELEZA UMUHIMU WA NISHATI YA UMEME KUPIKIA
*Ni katika muendeleo wa vikao kazi kati ya TANESCO na Madiwani Wilaya ya Kahama
*Awataka Madiwani kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi wa maeneo yao
Katika kuhakikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia inatekelezwa kwa vitendo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Bi. Glory Absalum, amewataka madiwani kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia nishati ya umeme kupikia ambayo ni salama kiafya, nafuu na inalinda mazingira.
Akizungumza Februari 17, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya TANESCO na madiwani wa kata 20 za Wilaya hiyo, Bi. Glory amesisitiza kuwa upatikanaji wa umeme ni fursa muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuendelea kutuletea miradi ya umeme inayorahisisha upatikanaji wa nishati. Leo hii kina mama wanaweza kupika kwa umeme wakiwa salama, wakitunza afya zao na mazingira. Matumizi ya umeme yanapunguza utegemezi wa kuni na mkaa na hivyo kulinda misitu yetu,” alieleza Bi. Glory.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Mhe. Benjamin Ngayiwa, amewataka madiwani kushirikiana kwa karibu na TANESCO kulinda miundombinu ya umeme ambapo amebainisha kuwa uharibifu wa miundombinu unaofanywa na watu wasio waaminifu ni moja ya sababu zinazoathiri upatikanaji wa huduma bora ya umeme.
Naye Meneja wa TANESCO Shinyanga , Mha. Khadija Mbaruku, amewashukuru viongozi hao kwa kuitikia wito wa kikao kazi hicho na kuahidi ushirikiano ili kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kwa wakati na kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo.
“Tunawashukuru kwa kutenga muda wenu kushiriki kikao hiki. TANESCO itaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha huduma ya umeme inaboreshwa, huku tukitoa kipaumbele katika taasisi za kijamii kama shule, zahanati na nyumba za ibada,” alisisitiza Mha. Khadija.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Mhe. Mataluma Kaniki, kikilenga kuwajengea uwezo madiwani kuhusu shughuli na mipango ya TANESCO katika maeneo yao.
TUME YA UCHUNGUZI YAONGEZEWA MUDA HADI APRILI 3, 2026
*DAR ES SALAAM:* MAMLAKA ya Uteuzi imeongeza muda wa siku arobaini na mbili (42) kuanzia tarehe 20 Februari, 2026 Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ili Tume iweze kukamilisha uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025 na kuitaka ikamilishe kazi na kuwasilisha Taarifa yake kabla au ifikapo tarehe 3 Aprili, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa katika gazeti la serikali Tume imeongezewa muda huo ili kutoa fursa na muda wa kutosha kwa kila mwenye taarifa, ushahidi au maoni, aliyepo nchini au nje ya nchi, kuwasiliana na Tume ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote, au taasisi yoyote, itakayokosa nafasi ya kusikilizwa.
Sababu nyingine za kuongeza muda ni pamoja na zifuatazo Wingi na mchanganyiko wa taarifa zilizokusanywa, na zinazoendelea kukusanywa, na Tume ambazo zinahitaji muda zaidi wa kufanyiwa uchambuzi wa kina, Tume kulazimika kutumia Wataalamu (experts) kutoka ndani na nje ya nchi wenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kisayansi, na uchambuzi wa kidijitali wa baadhi ya taarifa na vielelezo kutokana na aina ya matukio na ushahidi uliokusanywa hadi sasa, na unaoendelea kuwasilishwa.
Sababu nyingine ni Tume kubaini mapengo kadhaa katika taarifa na vielelezo vilivyokusanywa hadi sasa hivyo kuhitaji kutafuta au kupata taarifa zaidi ili kukamilisha ushahidi kwa kila hoja inayohusika, Kutoa fursa kwa wadau wachache muhimu ambao kwa sababu mbalimbali bado hawajafika mbele ya Tume, licha ya kupelekewa mialiko zaidi ya mara moja.
Taarika hiyo imewataja wadau hao kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa dini, viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi na Wingi wa wananchi wengine wanaoendelea kufika mbele ya Tume kuwasilisha taarifa, ushahidi na ushauri wao.
Kutokana na fursa hiyo ya Tume kuongezewa muda Tume kupitia Mwenyekiti wake Jaji Othuman Chande inatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuwasilisha ushahidi kwenye Tume kwa kutumia njia zote zilizokuwa zimeainishwa awali ambazo ni majadiliano ya ana kwa ana, mawasilisho ya maandishi (written submissions) kwa njia ya posta au tovuti maalumu ya Tume; barua pepe; ujumbe mfupi wa simu (SMS); kujaza dodoso maalumu kwenye mtandao (www.tume.uchunguzi.go.tz), au kwa kupitia mitandao mingine ya kijamii.
Pia tume hiyo imetoa wito maalumu kwa baadhi ya viongozi wa dini, viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi ambao wamepewa mialiko na Tume lakini bado hawajafika mbele ya Tume kutumia fursa hii kufika au kuwasiliana na Tume kutoa mchango wao katika uchunguzi unaoendelea kwa manufaa ya wananchi, wadau na nchi kwa ujumla.
Taarifa hiyo pia kupitia Gazeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaeleza Umma umuhimu wa kuendelea kuipa Tume ushirikiano ili kuiwezesha kukamilisha kazi yake ya uchunguzi. Kama ilivyokuwa mwanzo, Tume itaendelea kufanya vikao vya wazi (public hearing) isipokuwa pale ambapo mashahidi kwa faida ya usalama wao hawapendi majina yao, sura na taarifa zao zitolewe kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa Mpango Kazi, Tume ilipaswa kuwasilisha Taarifa kabla au ifikapo tarehe 20 Februari 2026 ikiwa ndani ya siku 90, ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 20 Novemba, 2025 mara baada ya kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais.
SIKU YA MSIKILIZAJI HABARI MAALUM MEDIA YALETA UCHUNGUZI WA MOYO BURE NGARAMTONI

Matroni wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sr. Flora Kasembe akitoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Msikilizaji yaliyoandaliwa na Habari Maalum Media na kufanyika Ngaramtoni jijini Arusha.
Na Mwandishi Maalumu – Arusha
21/2/2026 Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na elimu ya afya kwa mamia ya wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Msikilizaji yaliyoandaliwa na Habari Maalum Media, yaliyofanyika Ngaramtoni mkoani Arusha.
Katika tukio hilo lililowakutanisha zaidi ya wasikilizaji 400 wa kituo hicho, wananchi walipata fursa ya kupima afya za mioyo yao, kupimwa viashiria mbalimbali vya hatari pamoja na kupewa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Matroni wa Wauguzi wa ALMC, Sr. Flora Kasembe alisema zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa limewafikia wananchi wengi ambao hawapati muda wa kufika hospitalini kwa uchunguzi wa afya.
Alisisitiza kuwa uchunguzi wa afya mara kwa mara ni muhimu katika kugundua matatizo ya kiafya mapema na kuanza matibabu kwa wakati hatua inayosaidia kupunguza madhara makubwa, gharama za matibabu na vifo vinavyoweza kuzuilika.
“Wananchi wengi hupata matatizo makubwa ya kiafya kwa kuchelewa kugundua magonjwa. Tunawahamasisha kujenga utaratibu wa kupima afya zenu mara kwa mara ili kuzuia madhara yanayoweza kuepukika”, alisema Sr. Flora.
Aidha Sr. Flora ambaye ni Afisa Muuguzi aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kambi maalumu za huduma za kibingwa zitakazofanyika bila malipo katika Hospitali ya ALMC, ikiwemo kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu watakayoifanya kwa kushirikiana na wataalamu kutoa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) tarehe 23-27/02/2026.
“Kambi nyingine ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo tutaifanya tarehe 27-28/2/2026 kwa kushirikiana na wataalamu wenzetu kutoka Shirika la Heart to Heart Association for Sustainable Develepment la nchini Misri”, alisema Sr. Flora.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma ya uchunguzi wa moyo walieleza kufurahishwa kwao na upatikanaji wa huduma za bure karibu na makazi yao huku wakisema imewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata ushauri wa kitaalamu bila gharama.
Ernest Mollel mkazi wa Ngaramtoni alisema huduma hiyo imekuwa ya manufaa makubwa kwa jamii kwani watu wengi hawana tabia ya kupima afya hadi wanapoumwa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, upimaji wa mara kwa mara ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwani husaidia kugundua vihatarishi mapema na kuwezesha kupata tiba na kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha kabla hali haijawa mbaya.
Kupatikana kwa huduma hizo ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kinga na uchunguzi wa mapema.
DKT.JAFO AWEZESHA ELIMU YA UFUNDI, AKABIDHI VYEREHANI VINNE CHUO CHA FDC KISARAWE-MZENGA
Taasisi ya Jafo Education Foundation imefadhili jumla ya vijana 51 kusoma katika Chuo cha FDC Kisarawe – Mzenga, kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi wa fani mbalimbali za ufundi.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi na kuzungumza na wananchi katika Kata ya Mzenga, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Mhe.Dkt. Selemani Jafo, amesema vijana hao 51 watatoka katika kata zote 17 za wilaya hiyo na taasisi hiyo itagharamia ada zao za masomo.
“Hii ni fursa muhimu kwa vijana wa Kisarawe kujipatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa, hasa katika kipindi hiki ambacho soko la ajira linahitaji wataalamu wenye ujuzi wa vitendo.”amesema Dkt. Jafo
Dkt.Jafo amesema kuwa Chuo cha FDC Kisarawe – Mzenga ni chuo kipya kilichojengwa wilayani humo na tayari kinatoa mafunzo katika fani mbalimbali zikiwemo ufundi magari, ushonaji, ujenzi, mapishi, umeme, kompyuta pamoja na mafunzo ya muda mfupi.
Aidha, Dkt. Jafo ameeleza kuwa tangu mwaka 2010 amefanikiwa kusaidia zaidi ya vijana 500 kutoka familia zenye changamoto kusoma katika ngazi mbalimbali, ikiwemo kidato cha tano, astashahada, stashahada na shahada.
Katika kuendeleza juhudi za kukuza elimu ya ufundi, tarehe 20 Februari, Dkt. Jafo kupitia taasisi yake amekabidhi msaada wa vyerehani vinne vya umeme katika chuo hicho, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa dhamira kuu ni kuwawezesha vijana katika fani za ufundi ili kujenga msingi imara wa ajira rasmi na zisizo rasmi, pamoja na kuongeza kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Kisarawe.
WAZIRI MKUU KUANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI ARUSHA FEBUARI 22 -24, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu ujio huo wa Waziri Mkuu mkoani Arusha
Na Happy Lazaro,Arusha .
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anatarajiwa kuwa na ziara ya Kikazi Mkoani Arusha kuanzia Februari 22-24, 2026, akitarajiwa kutembelea na kukagua miradi sita yenye thamani ya shilingi Bilioni 194.2 kwenye Wilaya za Arumeru, Arusha na Longido pamoja na kuzungumza na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake leo Jumamosi Februari 21, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amesema Waziri Mkuu kesho Jumapili ataweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa bweni la kisasa la Chuo kikuu cha Kimataifa cha sayansi cha Nelson Mandela, kukagua upanuzi wa Miundombinu ya Hospitali ya Oltrumet pamoja na kuzungumza na wananchi eneo la Ngaramtoni.
“Tarehe 23, Mhe. Waziri Mkuu atakuwa Wilaya ya Longido na atatembelea na kupokea taarifa ya mradi mkubwa wa maji Kata ya Sinya, atazindua mradi wa upanuzi wa shule ya Sekondari Sinya iliyopanuliwa na kuwa na Kidato cha tano na sita na baadae kutembelea kituo cha utoaji wa huduma za Pamoja (One stop Border Post), Namanga na kisha kuzungumza na wananchi kwenye Viwanja vya shule ya msingi Namanga.”
amesema CPA Makalla.
Aidha CPA Makalla amewaalika wananchi wote kushiriki katika ziara hiyo, na kusema kuwa kwa siku ya tatu Mhe. Waziri Mkuu atafanya ziara yake Wilaya ya Arusha akitarajiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo Kikuu cha mabasi Jiji la Arusha eneo la Bondeni City, kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa soko la Kilombero pamoja na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara kwenye eneo hilo la soko Jijini Arusha.
PROF. SHEMDOE AELEKEZA MAGARI 14 YA USIMAMIZI WA MIRADI YA TACTIC KUFANYA KAZI ILIYOKUSUDIWA
Na OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaelekeza Mameneja na waratibu wa Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kuhakikisha magari 14 aliyoyakabidhi yanakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa ya usimamizi wa mradi huo ili wananchi wanufaike na barabara, masoko na stendi zinazojengwa kupitia mradi huo.
Prof. Shemdoe ametoa maelelezo hayo leo Februari 21, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo kwa Mameneja wa TARURA wa Miji 12 ya kundi la kwanza la Mradi wa TACTIC, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Millenium Tower Kijitonyama, Dar es Salaam.
“Magari haya yamenunuliwa kwa fedha za umma, hivyo yatunzwe na yakatumike kwa kazi za usimamizi wa mradi wa TACTIC na si nyinginezo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewata wakandarasi walio kwenye maeneo ya utekelezaji wa miradi ya TACTIC, kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia mikataba waliosaini ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, na kuongeza kuwa Serikali haitosita kusitisha mikataba inayosuasua kwa mujibu wa sheria na vipengele vya mikataba husika.
Prof. Shemdoe amesema Serikali haina changamoto ya kukosa fedha za utekelezaji miradi, kwani pindi mkandarasi akiwasilisha hati ya maombi ya malipo analipwa kwa wakati, hivyo hakuna sababu ya wakandarasi kushindwa kukamilisha na kukabidhi miradi kwa wakati.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Albert Kyando ameishukuru Serikali kwa kuwakabidhi magari yatakayowawezesha kusimamia miradi ya TACTIC kwa karibu na kuahidi kuwa watayatunza kama Prof. Shemdoe alivyoelekeza kwa maslahi ya umma na taifa.
Naye, Mmoja wa Madereva waliokabidhiwa magari hayo kutoka Jiji la Arusha Bw. Joshua Magati, amesema watayatunza magari hayo kama alivyoelekeza Prof. Shemdoe, na kuongeza kuwa watazingatia muda wa kuyafanyia ukaguzi na matengenezo pamoja na kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa ya usimamizi wa miradi ya TACTIC.
Friday, February 20, 2026
Oryx Gas Waja na Promosheni Maalum ya Mfungo


NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Akizungumza leo Februari 20,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo Meneja Masoko na Mauzo wa Oryx Gas Tanzania Shaban Fundi amesema huu ni mwezi wa kujitafakari ,kushirikiana ,kujitolea na zaidi ya yote kuunganisha watu wote.
“Ili kuunga mkono wateja wetu katika kipindi hiki maalum tunatoa bei ya promosheni kwenye mitungi yetu mipya ya kilo sita itauzwa kwa Sh.37000 nchi nzima hadi Zanzibar.”amesema Fundi
Pia amesema mbali ya kupunguza bei katika kipindi hiki cha Ramadhan na Kwaresma wateja wao watakaonunua au kujaza gesi kwenye maduka maalum ya Oryx na Mangi Shop watapokea zawadi ya futari papo kama ishara ya shukrani yao kwao.
Akizungumza kuhusu gharama za mtungi wa kilo sita amesema mpaka unafika nchini Tanzania gharama yake haipungui Sh.80,000 lakini Oryx katika soko mtungi huo unapatikana kwa Sh.40000 na kwa sasa tumetoa promosheni mpaka Sh.37000.
“Oryx Gas tunashusha bei kwa ajili ya kuiwezesha jamii iweze kutumia nishati safi ya kupikia.Pia tunaishukuru Serikali kwa mfano sasa hivi tunamsamaha wa kodi katika mitungi pamoja na jitihada nyingine wanazochukua.
-“Hata hivyo tunaomba Serikali iendelee kuangalia katika maeneo mengine ili kuhakikisha kwamba gesi pamoja na mtungi bei yake inakuwa chini ili wananchi waweze kupata kwa bei nafuu.Kwafanya hivyo Oryx Gas kwa kushirikiana na Serikali tunaweza kufanikisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi wengi zaidi.”
“Kuhusu gharama ukilinganisha mkaa na kuni bei yake iko juu zaidi ya nishati safi ya kupikia kwani kwa familia ya kawaida kwa siku moja inatumia kopo moja la mkaa ambalo linauzwa Sh.2000 hivyo kwa mwezi ni Sh.60,000 wakati mtungi wa gesi ya oryx wa kilo 6 ni Sh.40,000.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema lengo la kampeni iliyozinduliwa kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi wq Ramadhan na Kwaresma ni muendelezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.
“Oryx Gas lengo letu kubwa ni kuendelea kuhamasisha nishati safi ya kupikia na mimi na timu yangu tumejipanga vema kuhakikisha tunaendelea kufanya kampeni za kuwezesha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.Wakati huu wa Ramadhan na Kwaresma tunawatakia mfungo mwema lakini wakati huo huo tukihamasisha matumizi ya nishati safi.”
Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Gesi kwa Ujumla Carloline Msokwa amesema kipindi hiki Waislamu na Wakristo wanaungana pamoja kuomba toba na ni kipindi ambacho familia zinakaa kufanya ibada na kuomba toba lakini pia ni wakati wa kupika chakula kizuri kwa ajili ya kufuturu.
“Kwahiyo Oryx Gas tumekuja na kampeni ya Pishi la kibabe ambapo familia zitakaa na kupika pamoja lakini pia Oryx tumetoa punguzo la bei ili kuwezesha wananchi kutumia gesi.Pia nitoe rai huu ni wakati wa Watanzania kuwa wamoja na tuliombee taifa letu.”
Thursday, February 19, 2026
UHUSIANO WA TANZANIA NA KOREA KUSINI WAZIDI KUIMARIKA
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba akiagana na Balozi
wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Eunje Ahn, baada ya mkutano kati
yao kuhusu ushirikiano wa maendeleo, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara
ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akiongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao chake na Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Eunje Ahn (hayupo pichani), kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedeck Mbise, kilichofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba akiongoza kikao kati yake na Balozi wa Korea Kusini nchini, Mhe. Eunje Ahn, kuhusu kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo mawili, kilichofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Eunje Ahn, akiahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati katika nyanja za maendeleo, wakati wa kikao na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, kilichofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akiipongeza Korea Kusini kwa mchango wake katika sekta za maendeleo nchini, wakati wa kikao na Balozi wa Korea Kusini nchini, Mhe. Eunje Ahn, kilichofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
………..
Na. Josephine Majura na Peter Haule, WF, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, amesema kuwa Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Korea Kusini katika sekta mbalimbali, kupitia nafasi yake kama mshirika wa maendeleo na rafiki wa karibu.
Dkt. Mwamba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Eunje Ahn, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jjini Dar es Salaam, ambapo mazungumzo hayo yalihusu namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa msaada wa kifedha kupitia mikopo nafuu na ruzuku, ambazo zimekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu na maendeleo nchini.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mwamba pia alitoa salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili kwa manufaa ya wananchi wa mataifa haya mawili.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Mhe. Eunje Ahn, aliahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika miradi ya kimkakati, ili kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanapatikana kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha Bw. Melckzedeck Mbise na mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Compact Energies: Nishati ya Jua Ni Chachu ya Mageuzi ya Uchumi Tanzania
Na Mwandishi Wetu KAMPUNI ya Kitanzania ya Compact Energies, inayojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa vifaa vya kisasa vinavyotumia n...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
Hapa mmoja wa watoto hao akiwa na kijana mwenzake mwenye miaka 18, wote wako sawa lakini yeye hawezi kuzungumza kama watu wa kawaida. Mama S...
-
Mwanamuziki toka Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo, Mbilia Bel akitumbuiza katika viwanja vya bunge mjini Dodoma jana. . Picha na Jube Tranqu...

.jpeg)
.jpeg)




























.jpeg)












