Monday, January 23, 2017

WAZIRI KAIRUKI AZINDUA AWAMU YA KWANZA YA OFISI YAKE KUHAMIA DODOMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki akizungumza na waandishi wa habari juu ya safari ya kuhamia Dodoma iliyoanza rasmi leo kwa kuhamisha vifaa vya ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa ofisi hiyo.Kushoto kwa Waziri ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro na Naibu Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki akizungumza na watumishi wa ofisi yake juu ya safari ya kuhamia Dodoma iliyoanza rasmi leo kwa kuhamisha vifaa vya ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa ofisi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Laurean Ndumbaro wakiuaga msafara wa magari yaliyobeba vifaa vya ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa ofisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakielekea Dodoma kwenye makao makuu ya nchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Laurean Ndumbaro na Naibu Katibu wa Ofisi hiyo Bi. Susan Mlawi wakifuatilia kwa makini uamishwaji wa vifaa vya Ofisi yao kabala ya kuondoka kwenda Dodoma leo hii. Picha na Daudi Manongi-MAELEZO.

Na Daudi Manongi-MAELEZO.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki amezindua rasmi safari ya awamu ya kwanza kwa kuaga msafara wa magari yaliyobeba vifaa vya Ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa ofisi hiyo kuelekea Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Kairuki alisema umefika wakati wafanyakazi wa Serikali kuanza safari ya kuamia makao makuu Dodoma ili kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli wakati wa Maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa.

“Kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama kiongozi na mratibu wa shughuli za Serikali alihamia Dodoma Mwezi Septemba 2016,Wizara nyingine zimeendelea na maandalizi ya kutekeleza azma hii ya serikali, nami leo napenda kutumia fursa hii kuuarifu umma wa watanzania kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekamilisha maandalizi ya kuhamia Dodoma na hivi punde vifaa vya kundi la kwanza vitaondoka kwenda Dodoma”,Aliongeza Mhe. Kairuki.

Amesema katika kundi la kwanza jumla ya watumishi 87 watahamia Dodoma na litahusisha uongozi wa Juu wa Wizara ukiwajumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Baadhi ya Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi, Maafisa Waandamizi na Watumishi wengine.

Katika hatua nyingine Mh. Kairuki alisema wale wote wanaohitaji kukutana na Waziri,Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wake wafike katika Ofisi zilizopo Dodoma na kwa masuala yote yanayohusuu Sera na Sheria za Utumishi wa Umma na Utawala wa Utumishi wa Umma kwa Ujumla yatatekelezwa Mjini Dodoma lakini.

Aidha masuala ya Mishahara,Uendelezaji rasilimali watu,Ukuzaji maadili,Anuai za jamii,Uchambuzi ushauri na Utendaji kazi na Huduma ya teknolojia ya habari na mawasiliano yataendelea kushughulikiwa na ofisi ya Dar es Salaam.

Alisema Ofisi yake itafunguliwa Rasmi Mjini Dodoma Tarehe 30 Januari 2017 na itakuwa katika Jengo la College of Humanities and Social Sciences katika eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma kama makao yake ya muda mpaka hapo itakavyoelezwa vinginevyo.

No comments: