Monday, January 09, 2017

MVUA YAWAATHIRI WANANCHI WILAYANI RUNGWE MKOANI MBEYA


Mkazi wa Kijiji cha Ndubi kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya, Julius Mwambola (kulia), akionyesha migomba iliyoangushwa kutokana na mvua iliyonyesha wilayani humo mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni mke wake Nabwike Swebe.
Migomba ikiwa imeanguka kutokana na mvua hizo.

Mwanahabari Dotto Mwaibale, akichukua taarifa ya athari ya mvua hiyo kutoka kwa mkazi wa Kijiji cha Ndubi, Ambokile Mwangosi.

Nyumba ya Kikongwe, Gwanaloli Ndapapa ikiwa imeezuliwa paa na mvua hiyo ya upepo.
Kikongwe Maria Kamendu (85), akiwa ameshika paa la nyumba ya jirani yake Gwanaloli Ndapapa iliyobomolewa na mvua iliyonyesha mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Ndubi wilayani Rungwe mkoani Mbeya na kuharibu migomba na baadhi ya nyumba.


Dotto Mwaibale, Mbeya

WAKAZI wa Vijiji vya Ndubi, Mpuguso Kata ya Kisondela Tarafa ya Pakati wilayani Rungwe mkoani Mbeya wameathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo ambayo imeezua baadhi ya mapaa ya nyumba na kuangusha migomba.

Akizungumza kuhusu tukio hilo mkazi wa Kijiji cha Ndubi, Ambokile Mwangosi alisema wamepata pigo kubwa kutokana na mvua hiyo iliyonyesha mwishoni mwa wiki kutokana na migomba mingi kuanguka hivyo kutishia tishio la njaa.

"Siwezi kuelezea kwa undani tathmini ya athari ya mvua hii lakini tumepata pigo kwani kaya nyingi migomba imeangushwa na mvua hiyo" alisema Mwangosi.Mkazi mwingine wa kijiji hicho Julius Mwambola alisema mvua hiyo imeangusha migomba yake 100 yenye thamani ya sh.250,000.

"Tumeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mvua hii kwani mimi binafsi migomba iliyoangushwa na upepo wa mvua hiyo ni zaidi ya 100" alisema Mwambola.Mkazi mwingine wa Kijiji cha Mpuguso kitongoji cha Nkuju, Tulinagwe Naswila alisema mvua hiyo imeangusha migomba yake 40 yenye thamani ya sh.200,000.

Alisema mvua hiyo ilianza kunyesha saa saba mchana na ilidumu kwa muda wa saa moja na kuleta athari kubwa ya kubomoa baadhi ya nyumba na kuharibu migomba."Mvua ilikuwa kubwa ambayoiliharibu migomba na kuezua paa za nyumba kadhaa na kubomoa nyumba ya mjane mmoja aliyemtaja kwa jina la Gwanaloli Ndapapa (85).

Jitihada za kumpata Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya ili kuzungumzia suala hilo zilishindikana baada ya kupigiwa simu mara kadhaa bila ya kupokelewa

No comments: