Monday, January 23, 2017

WANANCHI WATAHADHARISHWA NA UTAPELI KUPITIA SIMU ZA MKONONI

 Kaimu Meneja  Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu Mwakyanjala akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu ulaghai kupitia simu za mkononi unaofanywa na matapeli katika kipindi hiki. Kulia ni Afisa Uhusiano wa TCRA Bi. Mabel Masasi
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) leo Jijini Dar es salaam. (Picha na Frank Mvungi-Maelezo).
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuwa makini na utapeli unaofanywa kupitia simu za mkononi.Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Meneja Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu Mwakyanjala wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Semu alisema kuwa kuna ongezeko la matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma pesa kwa simu za mkononi hivyo Mamlaka na vyombo vya usalama vinashughulikia suala hilo.“Usitekeleze maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu hata kama yanatoka kwa mtu unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba nyingine ili kuthibitisha’’ alifafanua Semu.

Alitahadharisha kuwa mtu akipokea taarifa kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kimakosa na kutakiwa kuzirudisha asifanye hivyo mpaka atakapojiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.

Akizungumzia matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mitandao, Semu alibainisha kuwa kwa miezi miwili ya Novemba na Desemba 2016 jumla ya fedha iliyopita kwenye mitandao ya simu za mkononi ni shilingi trilioni 13.07 hali inayothibitisha ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mitandao hapa nchini.

Alitaja makampuni yaliyohusika na takwimu za miamala hiyo kuwa ni Zantel (EASY PESA), Tigo (TigoPesa), Vodacom (M PESA), Airtel (Airtel Money) na Halotel (HALOPESA).

Aidha aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi kuhusu matapeli na kuwasilisha malalamiko yao ya huduma za mawasiliano kwa TCRA kupitia sanduku la posta 474 Dar es salaam au wafike kwenye ofisi za TCRA zilizo karibu au wapige simu namba 0784 558270, 0784 558271 na barua pepe (malalamiko@tcra.go.tz)

No comments: