Wednesday, January 04, 2017

RC Gambo akutana na wadau wa Elimu

rc1
rc2Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akishirikiana na wataalamu kuweka mitambo sawa kwa ajili ya wadau wa Elimu kuwasilisha taarifa.
rc3Viongozi wa Halmashauri ya Ngorongoro wakifuatilia Kikao cha Wadau wa Elimu
rc4Wadau wa Elimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karatu
rc5Kaimu Afisa Elimu Mkoa Emmanuel Mahondo akiwasilisha taarifa ya Elimu Mkoa wakati wa Kikao cha wadau wa Elimu kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
…………………………………………………………………………
Nteghenjwa Hosseah, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amewataka wadau wa elimu kuunganisha nguvu zao katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili kufikia malengo ya Serikali ya ufaulu wa asilimia 80 kila wilaya.
Gambo ametoa wito huo katika kikao chake na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri ,Maafisa Elimu wa Shule za Sekondari na Msingi pamoja na wadau wengine wa Elimu mkoani hapa.
Alisema ili kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa(BRN) yanayotaka ufaulu katika ngazi ya Elimu ya Msingi na Sekondari kufikia asilimia 80 lazima kuwepo na vifaa vinavyohusika kwa ajili ya  kufundishia na kujifunzia.
“Katika kuangalia elimu kwa mapana yake, hatuna budi kuwajengea uwezo walimu wetu kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapa motisha badala ya kuwaacha na elimu waliyoipata Chuoni pekee,” alisema Gambo
Pia aliagiza Halmashauri zote za Mkoa huu kununua Mashine za kufyatulia matofali tambazo zinapatikana kwa gharama nafuu kutoka shirika la viwanda vidogo (Sido) ili kurahisisha zoezi la ufyatuaji wa matofali kwa matumizi ya Shule.
Aliwataka Wakuu wa Wilaya Mkoani hapa kuona namna wanavyoweza kuwashirikisha wananchi kuchangia nguvu zao katika kufyatua matofali mara baada ya halmashauri kukamilisha ununuzi wa mashine za kufanyia kazi hiyo toka Sido.
“Uchakavu wa majengo na upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na vyoo imekua ni changamoto ya muda mrefu katika Sekta ya Elimu lakini viongozi mkifanikiwa kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu kazi katika miradi ya Elimu itasaidia kukarabati na kukamilisha ujenzi wa miundombinu kwa wakati muafaka hivyo kuboresha upatikanaji wa Elimu bora kwa watoto wetu”.
Naye kaimu Afisa Elimu mkoa wa Arusha, Emmanuel Mahondo amesema hali ya elimu imekua ikiimarika kwa ufaulu kuongezeka na kuwa katika mkoa wa Arusha ni halmashauri za Arusha Jiji na Arusha DC ndizo zilifikia viwango BRN.
Kikao hiki na wadau wa Elimu ni muendelezo wa vikao vya Mkuu wa Mkoa wa Arusha  pamoja na wadau wa sekta mbalimbali katika Mkoa huu kujadili changamoto na kuona namna ya kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.

No comments: