KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TASAF KISIWANI PEMBA.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angellah Kairuki akikagua bidhaa zilizotengenezwa na vikundi vya walengwa wa TASAF  
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angellah Kairuki akikagua bidhaa zilizotengenezwa na vikundi vya walengwa wa TASAF 

  Matuta ya kuzuia maji chumvi ,upandaji wa mikoko na uchimbaji wa mitaro ya maji ni Moja ya Miradi iliyojengwa kwa ufanisi Mkubwa.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angellah Kairuki akipata maelezo mbalimbali alipokuwa akikagua bidhaa zilizotengenezwa na vikundi vya walengwa wa TASAF

Na Estom Sanga - Pemba.

Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala Bora na Serikali za Mitaa imetembelea miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- Unguja na Pemba na kuridhishwa na hatua ya Maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wake  kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba akizungumza na wananchi wa shehia ya Ndagoni Kisiwani Pemba baada ya kukagua ujenzi wa tuta la kuzuia maji chumvi ya baharini yasiathiri mashamba ya wananchi, ametaka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kutumia fursa ya Mpango huo kupunguza kero ya umaskini.

Ametoa Mfano wa Miradi iliyojengwa kwa ufanisi kuwa ni pamoja na matuta ya kuzuia maji chumvi ,upandaji wa mikoko, uchimbaji wa mitaro ya maji ,uundwaji wa vikundi vya kuweka akiba, na ujenzi wa vyumba vya madarasa na zahanati miradi iliyotekelezwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini kwa utaratibu wa ajira ya muda kisiwani Unguja na Pemba.

Kwa kutengeneza matuta ya kuzuia maji ya chumvi, walengwa hao wa TASAF wameweza kuokoa zaidi ya hekta 200 za mashamba ya mpunga katika shehia ya Ndagoni kisiwani Pemba kwa njia ya ushiriki kwenye ajira ya muda .

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menenjimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema serikali inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli za TASAF ili kuziboresha zaidi kwa manufaa ya wananchi.

Aidha Waziri huyo ameiagiza TASAF kuviimarisha zaidi vikundi vya kuweka akiba na  kuwekeza vipatavyo 876 kwenye shehia 78 vilivyoundwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kisiwani humo kwa kuvipatia nyenzo muhimu hususani elimu na vitendea kazi ili vikundi hivyo viwe endelevu.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara mbunge wa Ukonga amesema mfumo wa kuwashirikisha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya kuibua na kutekeleza miradi unaotumiwa na TASAF umeamusha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za Maendeleo na kutatua kero zinazowakabili badala ya kuitegemea serikali pekee.

Wakitoa ushahuda wa namna wanavyonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika shehia ya Ndagoni na Shidi kisiwani Pemba ,baadhi ya walengwa wa Mpango huo wamewaambia wajumbe wa kamati hiyo ya bunge kuwa uwezo wao wa kuhudumia watoto hususani wanafunzi umeongezeka na hivyo kuboresha mahudhurio yao shuleni na hata kwenye vituo vya afya ili kutimiza masharti ya Mpango.

Hata hivyo baadhi ya walengwa hao wamesema kwa sasa wanakabiliwa na soko la bidhaa wanazozalisha hususani mboga mboga kutokana na ongezeko la bidhaa hiyo kwenye maeneo yao.Mpango wa Kunusuru Kaya masikini unaotekelezwa na TASAF nchini kote pia  umeweka mkazo katika  shughuli za usalishaji mali kwa walengwa ili waweze kukuza kipato .

Zifuatazo ni picha za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala Bora na Serikali za Mitaa wakati wa ziara yao kisiwani Pemba kukagua miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF.  

Comments