Sunday, December 26, 2010

Rais Kikwete amteua Jaji Mkuu mpya


TAARIFA YA IKULU
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Jaji Mohamed Chande Othman kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, kuanzia tarehe 28 DIsemba, 2010.

Jaji Othman anachukua nafasi ya Jaji Augustino Ramadhani anayestaafu kwa mujibu wa sheria tarehe 27 DIsemba, 2010.
Kwa sasa Jaji Othman ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa na pia ni mtaalamu binafsi juu ya hali ya Haki za Binadamu huko Kusini mwa Sudan, hadi mwezi Agosti 2011.

Jaji Othman alizaliwa tarehe 1 Januari, 1952, ana shahada ya kwanza ya Sheria (LLB) ya Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na Shahada ya Uzamili (MA) kutoka katika Chuo Kikuu cha Webster, Geneva-Uswisi.

Amewahi kuwa Makamu wa Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Rwanda huko Arusha na amewahi kushika nafasi sawa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali huko Timor Mashariki.

Jaji Othman pia, amewahi kufanya kazi ndani na nje ya nchi katika Mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kama vile Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Jaji Othman ataapishwa kesho tarehe 27 Disemba, 2010 katika viwanja vya Ikulu saa 4:00 asubuhi.

Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi
Ikulu
Dar es Salaam
26 Disemba, 2010

1 comment:

Anonymous said...

Just popping in to say nice site.