Monday, December 06, 2010

Teknolojia ya digitali yatinga mahakamani



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, akizinduwa mfumo wa kurekodi mashauri mahakamani kwa kompyuta na Tovuti ya Mahakama katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es salaam leo.

******************************************************



HATIMAYE Mahakama ya Tanzania imeanza rasmi kutumia teknolojia ya kisasa katika kuendesha shughuli zake, baada ya kuzindua mfumo mpya wa kuweka kumbukumbu za mashauri mbalimbali kwa kutumia kompyuta.
Mfumo huo wa digitali ulizunduliwa jana na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Sambamba na mfumo huo, mahakama pia imezindua tovuti yake ambayo itakuwa na taarifa mbalimbali kuhusu sheria zinazotumika nchini, hukumu za kesi za kuanzia mwaka 1979 na taarifa nyingine kuhusu kesi zinazoendelea mahakamani.
Kutokana na kuzinduliwa kwa mfumo huo sasa majaji wa Mahakama Kuu na wa Mahakama ya Rufani hawatalazimika kuchukua kumbukumbu za mwenendo wa kesi mbalimbali kwa kuandika kwa mikono na badala yake kazi hiyo itafanyika kwa kutumia kompyuta maalum.
Katika mfumo huo mwenendo wa kesi utakuwa unaingia kwenye kifaa maalumu cha kuhifadhia sauti kwenye kompyuta na baada ya dakika tatu sauti hizo huanza kuchapwa na wataalumu na kuwekwa katika maandishi.
Kwa kuanzia, mfumo huo utaanza kutumiwa na majaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu Dar es Salaam kabla ya kuziunganisha kanda nyingine 14 ikiwa ni pamoja na mahakama za chini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Dk Bilal alisema matumizi ya teknolojia hiyo yataharakisha usikilizaji wa kesi, lakini yatajenga mazingira mazuri kwa wawekezaji nchini.
Dk Bilal alisema ni matakwa ya haki na katiba ya nchi kuwa kesi zimalizike katika muda muafaka, lakini zimekuwa hazimaliziki mapema na kusababisha mahakama kulalamikiwa kwa kuchelewesha kumaliza kesi mbalimbali.
Aliitaka mahakama kutumia sheria kwa ufanisi na kwamba kasi katika kuhitimisha kesi imaanishe upatikanaji wa haki badala ya kuzua mashaka.
Badala ya kuahirisha kesi mara kwa mara, Dk. Bilal aliitaka mahakama kuhakikisha kuwa kesi zinaeneshwa kwa kasi, kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuhitimishwa kwa haki na usawa.
“Wafanyabiashara na wawekezaji wanavutiwa kuwekeza katika nchi ambazo utekelezaji wa mikataba ni rahisi kwa maana kwamba gharama za kufungua mashauri ni za chini na kesi kuendeshwa kwa haraka,” alisema Dk. Bilal .
Alisema matarajio ni kwamba kampuni ambazo zina matatizo ya kisheria katika shughuli zake za kibiashara, lazima yaweze kutatuliwa haraka ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma wa kampuni hizo.
Dk. Bilal alisisitiza kwamba haki za binadamu na katiba yetu zimejenga mazingira ya haki na usawa katika usikilizwaji wa mashauri na kwamba mahakama ndio yenye jukumu hilo.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Jaji Mkuu Agustino Ramadhani alisema mahakama imekuwa ikilalamikiwa kwa kuchelewa kumaliza mashauri kutokana na kutumia zaidi mfumo wa uchukuaji wa kumbukumbu unaotegemea kuandika kwa mkono tu.
Alisema kuzinduliwa kwa mfumo huo mpya wa kiteknolojia kutawawezesha majaji kuepukana na mfumo wa kizamani na hivyo kuharakisha uhitimishwaji wa kesi.
Jaji Ramadhani alisema faida kubwa ya mfumo huo ni kumwezesha Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi kujua kila kinachofanywa na kila jaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu.
Imeandikwa na James Magai wa Mwananchi

No comments: