Bambaga kuzikwa Musoma kesho



MAZISHI ya aliyekuwa mchezaji wa zamani soka wa Tanzania, Nico Bambaga yanatarajia kufanyika kesho nyumbani kwao Musoma mkoani Mara.

Bambaga alifariki dunia usiku wa Jumatatu katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam, alikuwa akisumbuliwa na homa ya mapafu.

Msemaji wa familia ya marehemu alisema jijini Dar es Salaam leo kuwa utaratibu wa mazishi ya mwanasoka huyo yalikuwa yakiendelea vizuri na mwili wake ulitarajiwa kusafirishwa jana kwa maziko ambayo yatafanyika kwa taratibu maalumu nyumbani kwao mjini Musoma.

"Kifo cha mpendwa wetu kwa kweli kimetushtua sana sisi kama wanafamilia na alikua na mchango mkubwa hivyo ameacha pengo kubwa kwetu ambalo si rahisi kuzibika kwa sasa.

Msiba huu si pengo kwetu tu bali kwa wanafamilia wote wa soka nchini kwani Nico alikuwa mchezaji wa kutumainiwa na ambaye aliweza kuichezea pia na timu ya taifa,"alisema.

Wakati wa uhai wake, Bambaga alizichezea Pamba ya Mwanza kabla ya kuhamia Yanga na baadaye Simba, Malindi ya Zanzibar, wakati huo akiichezea pia Taifa Stars. Imeandikwa na Jessca Nangawe.

Comments