WATU watatu wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Mara, wawili
wanachama wa Chadema na mmoja wa CCM akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kushambuliana katika Mtaa wa Kigera mjini Musoma.
Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kusababishwa na ukosefu wa uvumilivu wa kisiasa, lilitokea Oktoba 11, mwaka huu, kati ya saa 1:00 na saa 2:00 usiku katika mtaa huo.
Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mara Benedictor Mwijarubi aliwataja majeruhi hao kuwa ni Mapambano Malima (30) ambaye amekatwa upande wa kushoto wa uso , Sele Mwita (27) amekatwa mkono na mguu, wakazi wa Kigera na wafuasi wa Chadema.
Alimtaja majeruhi aliyechini ya ulinzi wa polisi kuwa ni Kapuru Charles (44) mwanachama wa CCM ambaye anadaiwa kukodiwa kufanya tukio hilo.
Muuguzi huyo, aliliambia Mwananchi kuwa majeruhi hao walikuwa wakitoka Kwangwa kuelekea mjini na kukutana na kundi lililokuwa na silaha za jadi na kuanza kurushiana maneno kabla ya kuwashambulia na kuwajeruhi vibaya watu hao.Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Robert Boaz hakutaka kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo.
“Nina jambo muhimu sana nalishughulikia ndiyo maana sijapokea simu yako, hilo suala naomba unitafute kesho nitakuwa na nafasi ya kulizungumzia, maana nimebanwa sana,”alisema na kukata simu.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Musoma kwa tiketi ya CCM, Vedastus Mathayo alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi, licha ya kupokea hakuweza kuzungumza lolote.
Naye Katibu Mwenezi wa CCM, Mkoa wa Mara Maximillian Ngesi alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema; “niko kwenye kikao nitakupa majibu,”alisema na kukata simu.
Habari kutoka kwa vyanzo mbalimbali zinadai wanachama wa Chadema walikuwa wakitoka kwenye mkutano na wanaCCM wakawavizia kwa ajili ya kuwapiga.
Mgombea wa Chadema jimbo hilo Visenti Josephat Nyerere alipotafutwa katika simu ya mkononi hakuweza kupokea licha ya kuita.
Mwananchi lilielezwa kuwa wagombea wote waliitwa na kamati ya ulinzi na usalama ili kuzungumzia suala hilo ambalo inalenga kuvunja amani nchini.
Hivi karibuni Chadema waliwatuhumu CCM kwa kuandaa vijana kwa ajili ya kufanya vurugu na walisema walikuwa wakifanya mazoezi mazito katika Shule ya Mshikamano na ofisi ya chama hicho.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara Ndegaso Ndekubali akijibu tuhuma hizo
alisema wao wanawafundisha vijana wao ukakamavu.
“Tunawafundisha ukakamavu ili kulinda mikutano yetu, lakini ili tukichokozwa tutajibu, maana Chadema ndiyo wamejiandaa kwa fujo,”alisema.
Kutokana na tuhuma hizo Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, Boaz alisema hakuna chama kinachoruhusiwa kuandaa vijana kwa ajili ya kulinda mikutano na kwamba polisi ndio wana wajibu wa kulinda mikutani na wala si vijana wa chama chochote. “Kazi ya ulinzi kisheria ni ya polisi na atakayeinua pembe tutaikata bila kuangalia chama ,”alisema. Imeandikwa na Anthony Mayunga-Mara. SOURCE MWANANCHI OKTOBA 12.
Comments