Friday, March 27, 2026

TBC Yawajengea Uwezo Washitiri Uzalishaji wa Vipindi

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bw. Gwakisa Mlawa akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 110 wa wadau wa elimu kwa umma (Washitiri), uliofanyika  katika ukumbi wa PAPU, Jijini Arusha, Machi 27, 2026

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano LATRA, Bw. Salum Pazzy, akitoa salamu za shukrani kwa TBC kwa niaba ya washitiri wengine wakati wa kufunga Mkutano wa 110 wa wadau wa elimu kwa umma uliofanyika  katika ukumbi wa PAPU, Jijini Arusha, Machi 27, 2026.
Baadhi ya Washitiri walioshiriki Mkutano wa 110 wa wadau wa elimu kwa umma uliofanyika  katika ukumbi wa PAPU, Jijini Arusha, Machi 23 - 27, 2026.

Adelina Johnbosco na Timothy Mwakyenda – MAELEZO

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limetoa mafunzo ya uandaaji bora wa vipindi kwa washitiri wa taasisi za umma nchini ili kuwajengea uwezo wa kutoa elimu kwa umma.

Washitiri hao kutoka vitengo vya mawasiliano vya wizara, taasisi, idara, mamlaka na mashirika ya umma wanahusika na utoaji wa taarifa za Serikali na utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa TBC, Bw. Gwakisa Mlawa, amesema ana imani mafunzo hayo yataongeza ujuzi na ufanisi kwa washiriki katika majukumu yao ya kila siku ya mawasiliano.

Amesema mafunzo hayo pia yatakuwa chachu ya maboresho ya maudhui yanayozalishwa, kutokana na maarifa waliyopata kupitia wataalamu waliobobea katika nyanja tofauti.

Mafunzo hayo yamejumuisha mada mbalimbali zikiwemo uongozi bora, uandaaji wa vipindi, matumizi ya akili unde (AI) pamoja na mbinu za utatuzi wa migogoro kazini.

“Mawasiliano siyo suala la kutoa na kupokea taarifa tu, bali ni kujenga taswira nzuri ya taasisi na taifa kwa ujumla,” alisema Bw. Mlawa.

Aidha, amesema TBC inaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuboresha utoaji wa huduma za habari na mawasiliano kwa wananchi akiwakaribisha wadau na wananchi kuendelea kuitumia TBC kama chombo muhimu cha utangazaji nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Bw. Salum Pazzy, akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake ameipongeza TBC kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamekuwa na manufaa makubwa kwa washitiri wote.

Amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kuzalisha vipindi vya elimu kwa umma kwa weledi na uzalendo. 

No comments:

TBC Yawajengea Uwezo Washitiri Uzalishaji wa Vipindi

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bw. Gwakisa Mlawa akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 110 wa wadau wa elimu k...