Tuesday, March 27, 2018

DC MATIRO APIGISHA KURA ZA SIRI KUBAINI WAUAJI WA WANAWAKE SHINYANGA VIJIJINI



Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano katika vyombo vya sheria ili kukomesha mauaji katika kata ya Salawe
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kufuatia kuibuka kwa taarifa za kuwepo kwa mauaji ya wanawake yanayoambatana na imani za kishirikina katika kata ya Salawe wilaya ya Shinyanga, mkuu wa wilaya hiyo Josephine Matiro amefanya mkutano na wananchi wa eneo hilo kwa ajili ya kutafuta chanzo na ufumbuzi kumaliza mauaji hayo.
Wananchi wa kijiji cha Songambele kata ya Salawe wanasema mauaji hayo yameanza kutokea tangu mwezi Desemba mwaka jana wakidai kuwa wanawake hukatwa mapanga ama kunyongwa na watu wasiofahamika ambao hutoweka na viungo vya siri vya wanawake wanaowaua. 
Inaelezwa kuwa katika kipindi cha  Januari Mosi hadi Machi 23 mwaka huu watu waliouawa katika kata hiyo ni wanne huku mauaji hayo yakihusishwa na imani za kishirikina.Kutokana na hali hiyo Mkuu wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo, alifika katika kata ya Salawe kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mauaji hayo kwa njia ya kuwashirikisha wananchi.
Aidha baada ya kuzungumza na wananchi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara,mkuu huyo wa wilaya aliagiza kufanyika/kupigwa kwa kura za maoni kwa ajili ya kuwabaini wahusika wa mauaji hayo na kuondoka na kura hizo kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
“Katika wilaya ya Shinyanga kuna kata 43, matukio ya mauaji ya namna hii yanatokea hapa,ni nyinyi hapa tu,sasa tumtafute mchawi na tumfanyie kazi,mkitaka kulimaliza tatizo hili ni  lazima mtupe ushirikiano,muwe tayari kufika mahakamani pale mtakapohitajika ,mjitokeze kutoa ushahidi ili wale watu msiwaone tena kwenye mitaa yenu”,alisema Matiro.
“Wananchi mmeendelea kulalamika kuwa kuna mauaji na kuitupia lawama serikali wakiwemo askari polisi kuwa wanapokea rushwa na kuwaachia huru watuhumiwa kumbe tatizo ni nyinyi kutotoa ushirikiano,naomba mbadilike, wafichueni wahusika ili tukomeshe tatizo hili kwani tunataka watu wawe salama na waishi kwa amani”,alieleza Matiro.
Aidha aliwataka viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla kuacha kupokea wageni na kwamba wageni wote wajitambulishe ili kujua wanafanya nini na wametoka wapi ili kukomesha
Wakizungumza mbele ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga, wananchi hao walisema matukio hayo yanatishia usalama wao na kusababisha waishi kwa hofu.
Walisema mbali na kuishi kwa hofu pia wanashindwa kufanya kazi zao za maendeleo na uzalishaji mali.Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Simon Haule aliyekiri kuwepo kwa mauaji katika kata ya Salawe alisema chanzo ni kuwania mali,migogoro ya mashamba,wivu wa mapenzi na imani za kishirikina.
Aidha aliwataka wananchi kupuuza uzushi kwamba kwenye kata hiyo kuwa kuna watu wanakata mapanga wanawake na kisha kuondoka na sehemu zao nyeti yakiwemo matiti. 
“Kwenye mkoa wa Shinyanga hakuna kitu kama hicho, isipokuwa kuna takwimu za wananchi 27 kuuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na sababu mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia (2016- Machi 2018) ambapo wanawake 12, na wanaume 15. 
Alitaja takwimu za mauaji mkoa wa Shinyanga kwa kuchambua kila mwaka ambapo mwaka (2016) waliuawa watu 12, wanawake Sita, Wanaume Sita, (2017) wanaume nane, wanawake wanne, mwaka huu (2018) kuanzia Januari hadi Machi wanawake wawili na mwanaume mmoja jumla watu 27.

No comments: