MRADI WA SOKO LA TUNGWI-SONGANI MANISPAA YA KIGAMBONI WAZINDULIWA,WANANCHII WAASWA KUITUNZA MIUNDO MBINU YAKE

 ​muonekano wa soko kwa nje​
 ​Mstahiki Meya mwenye suti ya kaki akiwa ameongozana na baadhi ya wananchi wakielekea kuzindua soko​
 ​Mstahiki Meya wa Manispaa ya kigamboni Mh. Maabadi Hoja akifungua kitambaa cha jiwe la msingi kuonesha uzinduzi rasmi wa soko​
 ​Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mh.Maabadi Hoja akisoma kibao cha uzinduzi mara baada ya kuzindua 
 ​wananchi na Meya wakisoma maandishi ya uzinduzi wa soko mara baada ya kuzinduliwa.​
 ​Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mh. Maabadi Hoja akikata utepe kuonesha ishara ya uzinduzi rasmi wa soko ​
 ​Mstahiki Meya akiwa ameongozana na wananchi wakikagua soko mara baada ya uzinduzi. 
 ​Baadhi ya wananchi walioshiriki uzinduzi wa soko​
 ​Mratibu wa TASAF Manispaa ya Kigamboni Bi. Janet Kacholi akisoma taarifa ya mradi kabla ya uzinduzi.​
 Mstahiki meya wa Manispaa ya Kigamboni Mh.Maabadi Hoja akizungumza na wananchi mara baada ya uzinduzi wa soko
Mwananchi na mfanyabiashara Bi. Rehema kambi akishukuru kufunguliwa kwa mradi huo na kuomba kuletewa miradi mingine ili wananchi wanufaike.

Wananchi wa mtaa wa Tungwi-Songani Kata ya Pembamnazi Manispaa ya Kigamboni wametakiwa kutunza miundombinu ya soko ili soko liweze kudumu kwa muda mrefu na kunufaisha wananchi wote kwa ujumla. 

Rai hiyo imetolewa jana na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mh.Maabadi Hoja alipokuwa akizindua mradi wa soko hilo ijumaa lililojengwa Mtaa wa Tundwi-Songani , alisema kuwa mradi huu umenza ujenzi muda mrefu tangu mwaka 2002, hivyo tunatarajia ukamilikaji wake utaleta maendeleo kwa wananchi wote wa Tundwi Songani na jamii nzima ya Kata ya PembaMnazi hivyo ni muhimu kuhakikisha unatunzwa. 

Alisema kuwa ulinzi uimarishwe wa miundombinu na kuhakikisha lengo lililokusudiwa la kuboresha mazingira na utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na wananchi wa Tundwi na kata ya Pemba Mnazi kwa ujumla linafikiwa. 

Akitoa taarifa ya mradi Mratibu wa TASAF Manispaa ya kigamboni Bi.Janet Kacholi alisema kuwa, mradi wa soko ni miongoni mwa miradi iliyoibuliwa na wananchi kupitia program ya TASAF, ambapo umelenga kutoa ajira kwa vijana kwa kupata fursa ya kuuza mazao mbalimbali na kuiwezesha Serikali kupitia Halmashauri kukusanya mapato kutokana na ushuru mbalimbali utakaotozwa kwa wafanyabiashara. 

Aliongeza kuwa hadi kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo jumla ya Tsh.91,858,842.24 zimetumika ambapo wananchi wamechanga kiasi cha Tsh.34.040.427.27 mchango wa TASAF ni Tsh.26,416,827.27 na Halmashauri ya Manispa ya kigamboni imetoa Tsh.31,401,587.7 ambazo zimekamilisha ujenzi wa meza za ndani baada ya Halmshauri ya Temeke kushindwa kutoa fedha za ukamilishaji kama ilivyoahidi wakati wa uibuaji wa mradi kabla ya kugawanywa. 

Soko lipo tayari kwa matumizi ambapo vizimba /meza 60 sawa na wafanyabiashara 60 wataweza kufanya biashara ndani ya soko hilo na eneo la nje kuzunguka soko linakadiriwa kuchukua wafanyabisahara 80 ikiwa watapangwa na kusimamiwa vizuri. 

Aidha Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Tundwi Bw. Mikdadi Simba alisema kuwa wananchi wamelipokea soko kwa mikono miwili na litawaletea maendelo kwa sababu wataweza kufanya biashara kisasa zaidi kwa kuzingatia mji unapanuka. 

Mfanyabiashara Rehema Kambi amesema tunashukuru kwa mradi huu wa soko kwani tunauhakika wa usalama wa bidhaa zetu hazitaweza kuharibiwa kwa mvua kama kipindi cha nyuma hivyo tunaomba Manispaa ituletee miradi mingine mizuri zaidi ya huu. 

Mwenyekiti wa mtaa wa Tundwi Bw.Rajabu Kihimbo aliongeza kuwa anaiomba manispaa ione namna ya kuwasaidia kwenye suala la umeme ili waweze kuimarisha ulinzi na wafanyabiashara waweze kufanya biashara hata nyakati za usiku. 

Uzinduzi wa soko umekuja mara baada ya kukamilika kwa ujenzi uliohusisha awamu mbili awamu ya kwanza ikiwa ni ujenzi wa jengo la soko , vyoo na nyumba ya kuhifadhia vifaa mbalimbali na awamu ya pili ujenzi wa vizimba. 

Imenadaliwa na 

Kitengo cha Teknolojia Habari na Mawasiliano 
Manispaa ya Kigamboni.

Comments