Wednesday, March 21, 2018

WAZIRI KABUDI AWATAKA WASAJILI WA VYETI VYA KUZALIWA MIKOA YA SIMIYU, MARA KUZINGATIA UMAKINI NA UZALENDO

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(wa tatu kushoto) akizindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati) akionesha nakala ya cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri huo na kutoa vyeti vya kuzaliwa, kwa mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akimkabidhi mkazi wa Manispaa ya Musoma cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake mwenye umri wa chini ya miaka mitano, mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa, kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA), Bi. Emmy Hudson akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika Uwanja wa Shule ya msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akitoa salama za Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Wasanii wa Kikundi cha Ngoma ya Asili cha Wagoyangi kutoka Maswa mkoani Simiyu wakitoa burudani wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mikoa ya Simiyu na Mara mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa hiyo uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.


Na Stella Kalinga, Simiyu

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Prof. Palamagamba Kabudi amewataka wasajili wa vyeti vya kuzaliwa kupitia mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwenye mikoa ya Simiyu na Mara, kufanya kazi hiyo kwa umakini na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha wanawasajili watoto wenye sifa.

Waziri Kabudi ametoa rai hiyo Machi 20 wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa, katika mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

“Mikoa ya Mara na Simiyu ina muingiliano mkubwa sana na wananchi wa nchi jirani hivyo wasajili wawe makini na watangulize uzalendo wakati wa kutekeleza mpango huu, tusisajili mtoto ambaye hahusiki na pale ambapo tuna mashaka kuwa mtoto huyo anaweza kuwa wa nchi za jirani, tutoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika ili hatua za kiusalama zichukuliwe” alisema Profesa Kabudi.

Amesema kuwa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano unafanyika bila malipo hivyo wasajili wasitumie kwa namna yoyote mpango huo kama fursa ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.Aidha, Waziri Kabudi ameahidi kutoa tuzo maalum kwa mkoa (kati ya Simiyu na Mara) utakaofikia asilimia 80 ya lengo la usajili kwa kipindi cha miezi miwili tangu usajili ulipoanza na wakati huo huo akawataka Viongozi wa Taasisi zote Umma kuvitambua vyeti vitakavyotolewa chini ya mpango huo kwa kuwa ni vyeti halali

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA) Profe. Hamis Dihenga amesema kupitia mpango wa usajili na kutoa vyeti kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, RITA inakusudia kusajili jumla ya watoto 735, 545 katika mikoa ya Simiyu na Mara kwenye vituo 463 (Mara) na Vituo 324 (Simiyu).

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe.Annarose Nyamubi akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe.Adam Malima amesema hadi sasa Mkoa huo umesajili jumla ya watoto 78, 625 na watahakikisha watoto wote wanaopaswa kusajiliwa wanasajiliwa ndani ya miezi miwili na baadaye kuendelea na usajili kwa watoto watakaozaliwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga, akitoa salamu za Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka amesisitiza wananchi kutambua umuhimu wa kuwasajili watoto wao ili waweze kutambulika, kupewa vyeti vya kuzaliwa na Serikali iweze kupata takwimu sahihi.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto (UNICEF) hapa nchini ambao ni miongoni mwa wafadhili wa mpango huu, Bi. Maud Droogleever , amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano wanasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Baadhi ya wananchi wa Mikoa ya Simiyu na Mara walioshirikia katika Uzinduzi wa Mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuleta mpango huo kwa kuwa umewarahisishia huduma ya kupata vyeti vya kuzaliwa kwa kuwasogezea huduma hiyo katika Ofisi za kata tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya

No comments: