Mkazi wa kata ya Kakonyo, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Bwana Faraja Kaijage akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii jinsi alivyopigwa na kuumizwa na wafugaji wa nchini Uganda kwa kosa la kukamata mifugo ya waganda iliyokula mazao ya wananchi wa Tanzania katika kijiji hicho mwaka 2016
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii wakikagua mpaka wa Tanzania na Uganda katika eneo la mto kagera
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii wakipanda juu ya jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda namba BP 30 katika kata ya Bugango wilaya ya Missenyi mkoani Kagera
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Dkt. James Mtamakaya akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii mipaka iliyopo kati ya Tanzania na Uganda
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii wakipanda juu ya jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda namba BP 30 katika kata ya Bugango wilaya ya Missenyi mkoani Kagera
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula (mwenye Tshirt ya njano) akiongoza Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii kushuka katika jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda namba BP 30 katika kata ya Kakunyu wilaya ya Missenyi mkoani Kagera
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii wakiwa mbele ya jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda namba BP 30 katika kata ya Bugango wilaya ya Missenyi mkoani Kagera (Picha na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
……………..
Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Nape Nnauye ameishauli Serikali kuboresha mipaka ya nchi kwa wakati ili kuondokana na migogoro inayojitokeza mara kwa mara kufuatia uvamizi wa wahamiaji kutoka nchi jirani.
Ameyasema hayo katika ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembea mipaka kati ya Tanzania na Uganda Wilaya ya Missenyi upande wa Tanzania Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Isingiro upande wa Uganda.
Nape amesema suala la kulinda mipaka ni muhimu hivyo ni vyema serikali kupitia Wizara ya Ardhi ikatenga fedha za kutengeneza barabara zilizoko mipakani ili kurahisisha ulinzi na usalama wa mipaka yetu na kuwezesha wakazi wa nchi hizi mbili kutambua mipaka ili kuepusha migogoro ya matumizi ya ardhi.
“Tumebaini kuwa kuingia kwa wananchi wa Uganda hasa kuleta mifugo yao katika lanchi ya Missenyi kunachangiwa na kutokuwepo njia maalumu na alama maalumu zinazotenganisha kati ya nchi na nchi hivyo watu wanaingia kupitia katika vichochoro visivyo rasmi na kuhatarisha amani kwa wakazi wa mipakani alisema Nnauye”
Kamati hiyo pia ilifanikiwa kufika katika vijiji vya Rwengiri, Bwenkoma na Bubale vilivyopo kata ya Kakunyu na kubaini kuwa baadhi ya alama zilizowekwa mpakani zimepotea hivyo wafugaji kutoka maeneo mbalimbali wanaendelea na shughuli za ufugaji bila kujali sheria.
Mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Denice Mwila amesema kuwa kamati ya ulinzi na usalama imekuwa ikikagua mipaka na kutatua changamoto mbalimbali hivyo kama barabara itatengenezwa katika mipaka yote ya Missenyi kazi ya kuwabaini waarifu itakuwa rahisi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula amesema kuwa mpaka sasa Wizara imepokea shilingi bilioni 4 za kuimarisha mipaka ambapo fedha zitakazotumika kuimarisha mpaka wa Tanzania na Uganda ni shilingi Bilioni 1.9 na shilingi Bilioni 2.1 kwa mpaka wa Tanzania na Kenya.
Aidha kupitia ziara hiyo ya kamati Dkt. Mabula ametoa wito kwa wawekezaji ambao ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao kuja kuyaendeleza kabla ya kuchukuliwa hatua za kuyagawa maeneo hayo kwa watu wengine.
“Kuna watu waliomba maeneo wakafuge lakini wameshindwa na baadhi wanayatumia kwa kazi ambazo hazieleweki huku baadhi wakiomba kufugia lakini wanayatumia kwa ajili ya kazi nyingine, nitawachulia hatua kama watashindwa kufanya kazi waliyoomba alisema Mabula.”
Akitoa taarifa kwa kamati hiyo, Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Dkt. James Mtamakaya amesema kuwa sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mabadiliko ya utawala na kwamba mpaka wa Tanzania na Uganda uliasisiwa na Uingereza na Ujerumani mwaka 1890, ulitafisiriwa mwaka 1902-1904 kwa kutumia marundo 15 ya mawe ambayo baadhi ya malundo hayo yapo mpaka leo.
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, ikiwa katika tarafa ya Missenyi ilitembelea kata za Kakunyu, Mutukula na vijiji vya Rwengiri na Lyengoma ambapo ni eneo huria la ranchi ya Missenyi ambalo lilitengwa na serikali kwa ajili ya ufugaji wa Ng’ombe katika ranchi hiyo na baadhi ya maeneo kuwa na wakazi wachache.
Akizungumza na wajumbe wa kamati ya Bunge mkazi wa kata ya Kakonyo, Wilaya ya Missenyi ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Bwana Faraja Kaijage amesema kuwa kuna changamato kubwa katika mipaka hiyo, ambapo kwa kumbukumbu zake mnamo Disemba 19, 2016 alipigwa na kuumizwa na wafugaji wa Uganda kwa kosa la kukamata mifugo ya waganda iliyokula mazao ya wananchi katika kijiji hicho.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Dennis Mwila amesema kuwa kuna migogoro katika baadhi ya vitalu huria vya Missenyi vilivyogawiwa mwaka 2006 inayosabishwa na ukosaji wa uzalendo kwa viongozi kwa kuwauzia ardhi wahamiaji haramu na baadhi ya vitalu kuleta mifugo aina ya Ng’ombe kutoka Uganda kwa malipo haramu.
Wilaya ya Missenyi ni Wilaya ilianzishwa mwaka 2007 ambapo imepakana na nchi ya Uganda upande wa Kaskazini, Wilaya ya Karagwe upande wa Magharibi na Wilaya ya Bukoba vijijini upande wa Mashariki ambapo pia Wilaya ina tarafa mbili, vijiji 77 na vitongoji 352.
Aidha upande wa mpaka wa Tanzania na Uganda Wilaya inapakana na Rakai na Isingiro zilizopo nchini Uganda ambapo mpaka una kilomita 110.7 na 0.5 ya umbali huo upo katika maji ya ziwa Viktoria.
Kwa upande wa idadi ya vituo vilivyo rasmi vya kupita watu ni vinne ambavyo ni Mutukula, Kilahya, Bugango na Kashenye na njia nyingine zisizo rasmi zipo mipakani takribani 20 vilivyo jirani na mpaka huo.
Comments