Watuhumiwa wa Ujangili, Peter Kabi (wa pili kulia) na mke wake Leonida Loi Kabi (wa tatu kulia) wakielekea kusomewa mashtaka ya kukutwa na meno 210 na mifupa mitano ya tembo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, wote wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Mtuhumiwa wa Ujangili, Peter Kabi (wa pili kulia) akielekea kusomewa mashtaka ya kukutwa na meno 210 na mifupa mitano ya tembo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa huyo na mke wake Leonida Loi Kabi (hayuko pichani) wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara hiyo anaeshuulikia Maendeleo ya Wanyamapori, Kanisius Karamaga.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa akizungumza na wanahabari katika moja ya ukumbi mahakamani hapo.
NA HAMZA TEMBA - WMU
...................................................................
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela Peter Kabi na Leonida Loi Kabi ambao ni wanandoa baada ya kukutwa na meno ya tembo 210 yenye uzito wa kilo 450.6 pamoja na mifupa mitano ya tembo.
Meno hayo yanayodaiwa kuwa ni sawa na idadi ya tembo 93 waliouwawa yalikutwa nyumbani kwa washtakiwa hao tarehe 27 Oktoba, 2012 eneo la Kimara Stop Over Jijini Dar es Salaam.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi amesema ametoa hukumu hiyo leo baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili Paul Kadushi na Elia Athanas ambao kwa pamoja umewatia hatiani washtakiwa hao.
Amesema katika kosa la kwanza kila mtuhumiwa atatumikia kifungo cha miaka 15 jela, kosa la pili na la tatu miaka 20 kila moja na kwamba hukumu hizo zitaenda kwa pamoja.
Akitoa ushahidi wa upande wa Jamhuri juu ya athari za ujangili nchini, Mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), aliyefahamika kwa jina moja la Lymo amesema idadi ya tembo hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa kwani sensa ya mwaka 2006 inaonyesha tembo walikuwa 1,034,000 tofauti na sesa ya mwaka 2012 ambayo ilionesha idadi hiyo kupungua na kufikia 43,000.
Alisema sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo kuongezeka na kufikia 50,000 ambayo ni matunda ya jitihada za Serikali katika kukabiliana na ujangili kwa kuongeza nguvu katika doria na mikakati mbalimbali ya kudhibiti ujangili.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo amesema, kila mtanzania anapaswa kujifunza kupitia hukumu hiyo kwa kuwa binadamu wote hujifunza kutokana na makosa na kwamba ni jukumu la kila mtanzania kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa.
“Rasilimali hizi ni zetu sote watanzania, sio za Serikali, sio za Wizara ya Maliasili na Utalii, sisi ni vibarua wenu, tuwalindie watoto wetu na wajukuu zetu hizi rasilimali, wasijekututukana huko mwishoni kama hawatakuta chochote wakalazimika kupanda ndege kwenda kuangalia vitu vilivyokuwa hapa hapa, watatutukana hatuna sababu ya kusubiri matusi” alisema Songorwa.
Comments