Sunday, February 05, 2017

WAFANYAKAZI WA SERIKALI WILAYANI HANDENI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO WAKIHITAJIKA KUTOA USHAHIDI MAHAKAMANI


 Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe akihutubia wananchi na viongozi mbalimbali kwenye maadhimisho hayo
 Afisa upelelezi Bw. Paul Kimaro akitoa hotuba fupi wakati wa maadhimisho ya sheria
 Mkuu wa Wilaya na wataalamu mbalimbali wakati wa wimbo wa Taifa.
 Waendesha mashtaka wa Wilaya ya Handeni Bw.Joseph Hamisi na Nzagalila Kikwelele  wakisikiliza hotuba wakati wa maadhimisho.
 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wikaya ya Handeni Bw. Noel Abel akisalimia wananchi.
 Wanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Amani Mangesho wa kwanza  kushoto na Bw. Joseph Vungwa wakijitambulisha kwa wananchi wakati wa maadhimisho
 Mh. Hakimu mkazi mfawidhi wa Wilaya ya Handeni na Kilindi Bw.Anorld kileo akitoa hutuba fupi wakati wa maadhimisho.
 Moja ya mwananchi akitoa hoja ya kupatiwa ufafanuzi.
Picha ya pamoja  Mkuu wa wilaya,  wataalamu  na wadau mbalimbali wa wanaosimamia Sheria.

Wafanyakazi wa Serikalini Wilayani Handeni wametakiwa kutoa ushirikiano kwa namna yoyote ile kama kuna eneo wanatakiwa kutoa ushahidi Mahakamani. Wametakiwa kuhudhuria mahakamani ili waweze kusaidia haki iweze kupatikana kwa wakati.
  
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alipokuwa akihutubia wananchi na wataalamu mbalimbali kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Handeni jana katika maadhimisho ya  siku ya sheria Nchini  iliyoandaliwa na Mahakama ya Wilaya mwaka 2017 yenye kauli  mbiu ya  “ umuhimu wa utoaji haki kwa wakati kuwezesha ukuaji wa uchumi”.

Gondwe alisema “amani na utulivu ndio matunda ya Haki, sehemu yeyote iliyokosa amani na utulivu basi lazima kuna haki imepokonywa” Kuli mbiu yetu inatukumbusha wadau wote ambao tunasimamia sheria kuanzia jamii ya kawaida , wataalamu, mawakili, wanasheria ,TAKUKURU, uhamiaji na magereza tuweze kufanya kazi kwa pamoja ili haki iweze kutendeka kwa wakati na kukuza uchumi wetu.

Aidha alieleza kuwa TAKUKURU, Magereza, Uhamiaji , Wanasheria na Mawakili wa Serikali na kujitegemea hawataweza kufanikiwa katika kupambana na Rushwa na kutoa haki kama Mahakama haitakuwa mdau mkuu katika hili. Alisema kuwa kwa kuliona hilo Mahakama imetoa elimu kwa  wananchi wiki nzima juu ya umuhimu wa utoaji wa haki kwa wakati kuwezesha ukuaji uchumi.

Mahakama yenyewe imefahamu  nafasi ya kusimama na kuweza kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha kwamba wananchi wanoishi Handeni wanapata haki mbali na changamoto mbalimbali zinazoikumba Mahakama hasa ukosekanaji wa watoa ushahidi hali inayopelekea kuchelewa kwa kesi na maranyingine kufungwa kwa kukosa ushahidi uliojitosheleza. Mwananchi anapodai haki lazima afahamu kuwa anao wajibu wa kufanya ili haki hiyo aweze kuipata, alisema Mh. Gondwe.

Aliongeza kuwa Serikali inafahamu mabaraza ya ardhi yanamatatizo, kwa kuliona hilo wanasheria wa Halmashauri ya Mji Handeni  wameanza kuelimisha viongozi wa mabaraza ya ardhi namna bora ya kusimamia kesi na wameelezwa  jinsi gani ambavyo wakienda kinyume mabaraza hayo yanaweza kuvunjwa kwani zipo taasisi nyingine kama TAKUKURU ambazo wanaweza kushughulikia wakiukaji wa kanuni za mabaraza ya ardhi kama watu wengine ambao sio waadilifu katika mifumo ya kiserikali. Viongozi wa Serikali wasitumie mifumo ya kiserikali kujihalalishia mapato yasiyo halali. Upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkurugenzi na wanasheria waeanza mikakati ya  kutoa elimu kwa mabaraza ya ardhi.

Mh. Gondwe Alieleza kuwa nyaraka nyingi za serikali zinatengenezwa bandia, alivitaka vyombo vinavyohusika na utoaji haki kuhakikisha wanahakiki nyaraka/vielelezo kutoka malaka husika ili viweze kuwa halali kwa utoaji wa haki.

Mwisho alizitaka taasisi za Serikali kufanya kazi na kuhakikisha zinawezesha Mahakama kwenye kesi ili kusaidia kesi hizo ziweze kuisha kwa wakati na kuokoa muda ambao wananchi wanapaswa kushiriki katika kukuza Uchumi mbali na jiografia ngumu ya Wilaya ya Handeni.

Mh. Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya Bw.Anorld Kileo alieleza kuwa Mahakama kama muhimili wa Serikali ndio chombo pekee kinachotoa Haki.  Dhima ya maadhimisho  haya inatutaka sisi kama watendaji wa Mahakama tuliokabidhiwa mamlaka ya kutoa haki tuweze kutoa haki kwa wakati ili kuwezesha jamii kuweza kuendelea na shughuli zao za Uchumi wa mtu binfsi na Taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya siku ya sheria Nchini  hufanyika kila mwaka wiki ya kwanza ya mwezi wa pili. Maadhimisho hayo yalijumuisha wadau  mbalimbali kutoka Halmashauri ya Mji na Vijijini Handeni wakiwemo Wanasheria, Mawakili, Idara ya Uhamiaji, Magereza, TAKUKURU na Polisi, yenye kauli mbiu ya  “Umuhimu wa utoaji haki kwa wakati kuwezesha ukuaji uchumi”.

Alda  Sadango
Afisa habari
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Post a Comment