Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akutana na Rais wa Tunisia

 Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete katika mazungumzo na Rais wa Tunisia Mhe. Beji Essebsi
 Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipokelewa na Rais Beji Essebsi katika Ikulu ya Tunisia
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na Rais Essebsi wa Tunisia mara baada ya kumkabidhi Ripoti ya Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu.

Rais Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amefanya ziara nchini Tunisia na kukutana na Rais wa Tunisia Mhe. Beji Caid Essebsi tarehe 17 Februari, 2017. Ziara hiyo ambayo ni muendelezo wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu ya kuwafikia viongozi wa nchi 14 za Afrika za kipaumbele katika kutekeleza mapendekezo ya Ripoti ya Kizazi cha Elimu (The Learning Generation).

Katika mazungumzo yao, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewasilisha kwa Rais Essebsi mapemdekezo ya ripoti ya Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu  na kuiomba Tunisia kujiunga katika mpango wa nchi za mstari wa mbele (pioneer countries) katika kufanikisha Kizazi cha Elimu ifikapo mwaka 2040. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu wa Tunisia Mhe. Neji Jalloul.

Kwa upande wake, Rais Essebsi wa Tunisia amemuhakikishia Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete uthabiti wa azma ya nchi yake kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu. Ameelezea utayari wa nchi yake kujiunga na mpango huo wa kufanikisha mapinduzi ya sekta ya elimu ndani ya kizazi kimoja ifikapo mwaka 2040.

Mbali na mkutano wake na Rais wa Tunisia, awali, Rais Mstaafu alikutana na kuwa na Mkutano na Waziri wa Elimu wa Tunisia na kutembelea Kituo cha Uendelezaji Teknolojia katika Elimu kilichoko Tunis na baadae kuzungumza na wanahabari kuhusu kazi za Kamisheni na Ripoti yake.

Comments