Rais apoke ripoti ya Epa kimyakimya

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo (Jumatatu, Agosti 18, 2008) amepokea rasmi ripoti ya uchunguzi wa upotevu wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje (External Payments Accounts - EPA) katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete amekabidhiwa ripoti hiyo na Mwenyekiti wa Timu iliyokuwa inafanya uchunguzi huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson P.M. Mwanyika.

Mwanasheria Mkuu huyo alifuatana na wajumbe wengine wa Timu hiyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hosea.

Rais amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Timu hiyo kwa kazi kubwa na ngumu lakini nzuri.

Rais, baada ya kuwa ameisoma na kuitafakari ripoti hiyo, ataitolea maamuzi katika siku chache zijazo, na taarifa rasmi ya maamuzi hayo ya Rais itatolewa kwa wananchi.

Timu hiyo iliundwa na Rais Kikwete Januari 9, mwaka huu, 2008 katika tangazo rasmi lililotolewa kwa waandishi wa habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Wakati anaunda Timu hiyo, Rais aliipa muda wa miezi sita kukamilisha kazi yake, ambayo ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa.

Rais aliunda Timu hiyo baada ya kuwa amepitia Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Mwaka wa Fedha 2005/06 za EPA katika Benki Kuu Tanzania (BOT), uliofanywa na Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young, kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kampuni hiyo ya Ernst and Young iliombwa na Serikali kuifanya kazi hiyo. Iliianza Septemba, 2007 na kumalizika Desemba, mwaka huo huo, 2007.

Rais Kikwete alikabidhiwa Taarifa hiyo Januari 7, mwaka huu, 2008 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Siku ya tatu, baada ya kuwa ameisoma na kuifanyia kazi, Rais aliitolea maamuzi Taarifa hiyo, ikiwa ni pamoja na kuunda Timu ya Mwanyika.


Imetolewa na

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

18 Agosti, 2008

Comments