Friday, September 28, 2007

Hayati Kaduma kuzikwa Iringa


Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Michuzi zinaeleza kuwa MSANII mkongwe wa sanaa za maonesho nchini, Mzee Godwin Zilaoneka Kaduma, aliyefariki dunia jana mchana kwa maradhi ya kupooza (stroke) anatarajiwa kusafirishwa leo Ijumaa kuelekea nyumbani kwake Bagamoyo na baadaye kijijini kwake Itamba, Iringa, kwa Mazishi.
Enzi za uhai wake marehemu mzee Kaduma aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa la Lugha ambayo kwa sasa imebadilishwa na kuwa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni.
Baada ya kustaafu Serikalini marehemu mzee Kaduma aliendelea na shughuli za sanaa akiwa kama kiongozi na mtendaji katika sanaa za maonesho ikiwamo ngoma na maigizo.
Alikuwa mwanzilishi wa Kituo cha Sanaa za maonesho Tanzania (TzTC) na Taasisi ya sanaa za maonesho Mashariki mwa Afrika (EATI) ambapo pia alikuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa asasi hizo.
Aliamua kupumzika kuzitumikia asasi hizo mwaka 2003, ambapo aliendelea na shughuli zake za kawaida za kufundisha masuala ya sanaa katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo akiwa kama mkufunzi mwalikwa katika Idara ya tamthiliya ambapo alikuwa akifundisha somo ya uandishi wa michezo ya kuigiza kazi aliyokuwa anaedelea kuifanya hadi kifo kilipomkuta.
Marehemu Kaduma pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Hakimiliki (Cosota) hadi kufa kwake, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi na uelewa kiasi hata kuamsha wasanii katika kuona umuhimu wa chombo hicho na kujisajili wao na kazi zao kwa wingi kuliko wakati wowote wa uhai wa Cosota.
Kwa mara ya mwisho, marehemu mzee Kaduma alifanya onesho akiwa msanii wa kujitegemea mwezi Juni mwaka huu, wakati wa semina maalum ya kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, iliyoandaliwa na Mfuko wa Utamaduni Tanzania ambapo alitamba na shairi la 'Naililia Tanzania'.
*KWA MUJIBU WA RATIBA ILIYOTOLEWA USIKU HUU NA KAMATI YA MAZISHI INAONESHA MWILI WA MAREHEMU MZEE KADUMA UTAAGWA ASUBUHI SAA 4 KATIKA HOSPITALI YA MUHIMBILI, KABLA YA KUPELEKWA NYUMBANI KWAKE BAGAMOYO AMBAKO UTAAGWA NA WAKAZI WA HUKO NA SAA NANE SAFARI YA KUMSAFIRISHA ITAANZA SAA 8 MCHANA KUELEKEA KIJIJINI KWAKE ITAMBA, IRINGA, KWA MAZISHI
MOLA AILAZE PEMA PEPONI ROHO YA MPENDWA WETU MZEE KADUMA
AMINA

No comments: