Thursday, September 06, 2007

Haya ya Hoyce na maoni yake kwa Miss Tanzania

AdhiaHoyce.
Yamesemwa mengi jamani wengine tukaamua kukaa kimya kuhusu huyu Miss Tanzania wetu leo nimepita mtandaoni nikamkuta mdau mmoja mwenye uchungu akisema hivi: msome kidogo
"NILIDHANI walioziacha fikra za Mwalimu ni viongozi wa CCM peke yao, kwa
hakika nilikuwa nimekosea sana. Jumamosi iliyopita wakati Watanzania wengine
walikuwa wanafurahia ushindi wa Taifa Stars dhidi ya The Cranes ya Uganda,
kuna kundi la Watanzania waliokuwa wananung'unika kwanini binti mwenye asili
ya Kihindi kachaguliwa kuwa Vodacom Miss Tanzania 2007.

Kwa vile Watanzania tuna mazoea ya kusahau mambo muhimu, hasa timu yetu ya
taifa inapocheza, nimeonelea nililete jambo lililotokea Leaders Club,
Kinondoni, Dar es Salaam mapema kabla ya mechi ya marudiano na Msumbiji.

Kama nilivyosema hapo juu kuwa mwanzoni nilipokuwa naliangalia suala la
"kuziacha fikra za Mwalimu" nilikuwa naangalia kwa mtazamo wa vyama vya
kisiasa zaidi, lakini baada ya kusikia mwitikio wa watu baada ya Richa Adhia
kuwashinda warembo wengine 25 na kutwaa taji hilo maarufu zaidi la urembo
Tanzania, nimejikuta nikihitimisha kuwa si viongozi wa CCM tu walioziacha
fikra za Mwalimu bali pia wananchi wa kawaida na wengine wenye nafasi kubwa
katika jamii ambao si tu wameziasi fikra hizo, bali pia bila haya wala
kusitasita wanatangaza hadharani hoja zao mbovu na zisizo na nafasi katika
Tanzania hii.

Sijui ni makosa ya nani au ni kutokana na sababu ipi kwamba Watanzania
tumeanza kuwa wabaguzi wa rangi. Kwa taifa ambalo lilimwaga damu yake
kuupinga ubaguzi wa rangi, na kutoa rasilimali zake kuwasaidia wapigania
uhuru, inaudhi na inatisha kuona kuwa leo hii bila hata aibu, tunatangaza
hadharani kuwa sisi ni wabaguzi! Gazeti moja liliandika kwa kichwa cha
habari kikubwa kuwa kitendo cha binti huyo wa Kitanzania kuchaguliwa ni
"aibu".

No comments: