Saturday, September 22, 2007

Balozi aitaka Tanzania ijisafishe



*Ni kuhusu tuhuma za BoT na suala la madini
*Aonya isipofanya hivyo itachelewesha kupata misaada
*Ashangaa nchi kuwa maskini wakati ina rasilimali nyingi

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Uholanzi imeeleza kukerwa na tuhuma za rushwa na ufisadi ambazo zinaendelea kujitokeza nchini dhidi ya viongozi mbalimbali, zikiwamo zinazoihusu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na nyingine zinazohusisha moja kwa moja upotevu wa rasilmali za umma huku serikali ikiwa kimya

Balozi wa Uholanzi nchini Karel van Kesteren alisema hayo juzi usiku wakati akiwakaribisha maofisa wapya wa ubalozi huo nchini ambao ni Mkuu wa Idara ya Uchumi, Steef van den Berg na Mirjam Tjassing ambaye ni afisa katika idara hiyo.

"Lakini, lazima nielezwe kwanza, kwamba ninaguswa sana na tuhuma zinazotolewa mara kwa mara kuhusu ufisadi. Ninaguswa zaidi na madai mengi ya ufisadi ambayo siku za karibuni yamekuwa yakiendelea kutolewa," alisema balozi huyo.

Kauli ya Balozi huyo ni ya kwanza kutolewa na ubalozi wa kigeni nchini baada ya vyama vya upinzani vitangaze tuhuma za viongozi mbalimbali wa serikali wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi.

Alisema licha ya hatua zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kuinua uchumi wa nchi kuwa za kuridhisha, lakini taarifa zinazohusu rushwa katika ujenzi wa Majengo pacha ya BoT, zinaichafua sifa ambayo nchi imeanza kujijengea.

"Tanzania inazidi kuingia katika nchi zenye uchumi wa kati, hilo linatia moyo, lakini ili iweze kufikia mahali hapo, inahitaji kuweka mazingira mazuri zaidi kiuchumi.

Alisema Tanzania inatakiwa kujenga mazingira ambayo sekta binafsi iweze kukua, kufanya kazi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuitaka serikali kujenga mazingira ambayo yatavutia wawekezaji kutoka nchi za nje, ikiwamo Uholanzi kuja na kufanya shughuli zao hapa.

"Tuhuma zinazohusiana na BoT (hasa Idara yake ya Malipo ya Nje, ambazo nasikia zimeanza kuchunguzwa kwa kazi inayofanywa na wakaguzi huru wa nje), pia naguswa mno na gharama halisi za ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo (BoT twin towers)," alisema balozi huyo.

Alisema majibu sahihi na kwa muda unaotakiwa kutoka serikalini, ndiyo yanayotakiwa kwani hayo ndiyo yatakayoweza kusaidia kuipa imani jamii ya wahisani wa kimataifa, serikali zao, kama ilivyo kwao Uholanzi, au hata mabunge, walipa kodi wao na hata wawekezaji hatua ambayo itaonyesha kuwa serikali (Tanzania) imekuwa makini, haina chochote cha kuficha katika hili.

Alisema kuchelewa kwa serikali kuchukua hatua kunaweza pia kuchelewesha utoaji wa ahadi na misaada mipya ambayo inatolewa na nchi wahisani, pia hili linaweza kuwakwaza wawekezaji

Balozi huyo aliongeza kuwa si rushwa kubwa kubwa tu inayoikera serikali yake, badala yake akaongeza kuwa ili kurejesha imani kwa wahisani, rushwa ya aina yoyote haina budi kuchukiwa na kisha kuchukuliwa hatua kali na za haraka.

Alionya dhidi ya maamuzi ya baadhi ya watu wenye uwezo kuelekea kupewa nafasi zaidi wakati mwingine kuliko maslahi ya maelfu ya watumishi ambao ajira zao zinahatarishwa kutokana vitendo hivyo vya rushwa au wakati mwingine ajira zao kupotea.

Balozi huyo, pia alieleza masikitiko yake kutokana na hali za maisha ya watu wengi nchini kuendelea kuwa duni huku wachache wakiendelea kuneemeka mwakati wananchi walio wengi wakiendelea kuishi katika hali ya umaskini wa kutisha.

Balozi huyo alieleza kuwa Uholanzi itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa Tamzania katika masuala ya maendeleo na kufahamisha kuwa mwaka huu, imetoa msaada unaofikia zaidi ya Euro milioni 80 (karibu dola za Kimarekani milioni 100) ambazo alisema sehemu kubwa imechangiwa kupitia katika bajeti ya serikali.

Hata hivyo, balozi huyo alieleza kuwa si jambo la kujivunia kwa Tanzania, kuona asilimia 40 ya bajeti inachangiwa na wahisani na washirika wa maendeleo.

"Lazima mtambue kuwa jambo hili haliwezi kuendelea daima. Ninaishauri Tanzania ianze kuangalia jinsi ya kujiondoa katika mtego huu wa kutegemea misaada, hasa kwa kusaka vyanzo vyake vya mapato. Licha ya ukweli kwamba mapato yanayotokana na kodi yanaongezeka, tunaipongeza serikali kwa mafanikio hayo, lakini hiyo bado haitoshi," alisema.

Balozi huyo alisema hiyo haitoshi kwa sababu uchumi wa Tanzania bado ni wa chini mno na kwamba nchi inatakiwa kuwa na mkakati wa kukuza uchumi wake haraka, ili ukuaji wa uchumi uwe zaidi ya asilimia sita au saba za sasa.

"Ukuaji huu wa sasa unatia moyo, lakini ili kupunguza kiwango kikubwa cha umaskini, ukuaji uchumi unapaswa uwe mkubwa na unaokwenda haraka. Hiyo, inatakiwa kuwa dira ambayo Tanzania haina budi kujiwekea, pamoja na jamii na iwe ya kuiweka katika uchumi wa kiwango cha kati ifikapo mwaka 2020," alisema.

Balozi huyo alieleza pia kuwa, ili kuchangia katika kukua na kuimarika kwa uchumi, sekta binafsi haina nudi kushirikishwa na kuhusishwa kikamilifu.

Alieleza faraja ya Uholanzi kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimewekeza kwa kiasi kikubwa katika Tanzania. Nchi nyingine ni, Uingereza, China, India na Afrika Kusini, katika sekta mbalimbali zikiwamo za kilimo cha maua, benki, utalii, mawasiliano na nishati .

Alishauri kuwa mapato yanayotokana na kodi hayana budi kuelekezwa katika sekta muhimu kama vile, elimu na afya, kuongeza na kuimarisha miundombinu. Akaongeza kuwa hilo ndilo ambalo Watanzania wanalihitaji zaidi kwa sasa.

Alifahamisha kuwa mambo hayo hayajafanyika katika Tanzania licha ya uwekezaji ambao umekuwa ukiendelea kufanyika na kushauri kuwa kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji nchini ili wawekezaji wanapoingia nchini wapate nafasi ya kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alionya kuwa wanachotaka kuona wawekezaji na wahisani ni kuona matunda ya fedha zao zinazoingizwa na kuwekezwa katika Tanzania badala ya kuendelea kuwaona watu wakiwa maskini wa kutupwa.

Aliwataka viongozi wa Tanzania kuwa tayari kujifunza kutoka nchi nyingine kama Kisiwa cha Mauritius, ambacho hakina madini kama dhahabu, gesi au mafuta, lakini kimepiga hatua kubwa kimaendeleo, kiasi cha wananchi wake kuwa na kipato kinachofikia dola za kimarekani 5,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na dola 350 kwa Watanzania. HABARI hii imetoka gazeti la Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Namuunga Balozi mkono. Baada ya serikali na chama tawala kutoa vitisho kwa watoa maoni mbalimbali, ingefaa kutoa ufafanuzi wa lawama ambayo inatupiwa ili kuondoa dukuduku kwa wananchi na dunia nzima kwa ujumla. Kinyume cha hapo,kunaonyesha kuwa hoja zilizotundikwa hadharani ni za kweli.