Monday, October 05, 2026

SERIKALI YATAKA MAKAZI YAENDANE NA KASI YA UKUAJI WA MIJI

 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi, Bw.Deogratius Kalimenze,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.

Afisa Mkazi wa Shirika la Makazi Duniani nchini Tanzania (UN-Habitat), Dkt. Grace Lubaale,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akiwa katika picha ya pamoja wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akiwa katika picha ya pamoja wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo “hayupo pichani)  wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo “hayupo pichani)  wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma.

Na Alex Sonna, Mzalendo Blog-DODOMA

SERIKALI imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata makazi salama, bora na yanayomudu gharama, huku ikisisitiza umuhimu wa upangaji wa miji, usalama wa milki na uwekezaji katika miundombinu ili kukabiliana na changamoto za ongezeko la watu na mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 5,2026 jijini Dodoma, ambapo amesema kuwa kasi ya ongezeko la watu na upanuzi wa miji inahitaji mipango madhubuti ya kuhakikisha maendeleo ya miji yanaenda sambamba na upatikanaji wa makazi bora na huduma muhimu.

“Serikali inaendelea na mchakato wa kuifanyia maboresho Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 ili iendane na mahitaji ya sasa, huku ikisisitiza kuwa sera hiyo inapaswa kutoa mwongozo wa kujenga makazi salama, himilivu na yanayomudu gharama kwa wananchi wa mijini na vijijini.”amesema Dkt. Akwilapo

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, vipaumbele katika kipindi kijacho vitajikita katika kurahisisha upatikanaji wa hati miliki na kuimarisha usalama wa milki, kuimarisha upangaji na usimamizi wa ardhi, kurasimisha makazi yasiyopangwa pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na taasisi za fedha kushiriki katika ujenzi wa nyumba bora na nafuu.

Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea na Mradi wa Uboreshaji wa Makazi ya Sinza, ambao umewekwa katika kundi la miradi ya kipaumbele ya kuboresha makazi mijini.

“Serikali imesisitiza kuwa  lengo ni kuipanga upya Sinza kwa kuzingatia mahitaji ya wakazi na uzoefu wa maboresho yaliyofanyika katika maeneo mengine ya Dar es Salaam, yakiwamo Samora, Kariakoo na Buguruni.”amesisitiza Dkt. Akwilapo

Aidha, ameeleza kuwa maboresho ya miundombinu ya usafiri, maji, umeme, masoko na barabara kupitia miradi mbalimbali ni sehemu ya juhudi za kujenga miji yenye huduma bora na inayoweza kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji.

Amesisitiza kuwa makazi bora yanapaswa kumwezesha mwananchi kuishi kwa usalama na heshima, kulea familia kwa utulivu na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Wakati huo huo,Dkt. Akwilapo,ametoa wito kwa mamlaka za miji na taasisi zinazohusika na maendeleo ya makazi kuchukua hatua mapema kukabiliana na athari za mvua kubwa na mafuriko, ikisisitiza umuhimu wa kupanga matumizi ya ardhi, kutunza mazingira na kujenga miundombinu inayostahimili majanga.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “Adequate Housing for All” (Makazi Toshelevu kwa Wote) yameitaka Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, vyuo, watafiti, mashirika ya kimataifa na wananchi kuunganisha nguvu kutoka kwenye mijadala na mipango kwenda kwenye utekelezaji, ili kuhakikisha Tanzania inajenga miji salama, jumuishi na endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi, Bw. Deogratias Kalimenze, amesema ukuaji wa kasi wa Tanzania na upanuzi wa miji umeongeza mahitaji ya nyumba, ardhi iliyopangwa, miundombinu na huduma za msingi, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kupata suluhisho la changamoto za makazi nchini.

“Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari kubwa kwa jamii, hivyo ni muhimu kujenga makazi yanayozingatia uwezo wa kustahimili changamoto hizo” amesema Kalimenze.

Pia amewataka wadau wote kutumia majadiliano hayo kubadilishana uzoefu na maarifa, kutengeneza suluhisho zinazofaa kwa mazingira ya Tanzania na kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora unakuwa jukumu la pamoja ili “hakuna mtu anayeachwa nyuma.”

Awali  Afisa Mkazi wa Shirika la Makazi Duniani nchini Tanzania (UN-Habitat), Dkt. Grace Lubaale, amesema makazi bora si suala la kuwa na paa pekee, bali ni msingi wa utu, afya, usalama, fursa za kiuchumi na maendeleo ya jamii, hivyo juhudi za kuboresha makazi zinapaswa kuangalia maisha ya watu kwa ujumla.

Amesema kasi ya ukuaji wa miji nchini inaongeza mahitaji ya nyumba, ardhi, huduma za msingi na miundombinu, hivyo kuna umuhimu wa kupanga ukuaji wa miji mapema, kuboresha makazi yasiyo rasmi na kuhakikisha wananchi wanapata ardhi na huduma muhimu kwa gharama zinazomudu. Amesema hatua hizo zitasaidia kujenga mitaa salama, iliyounganishwa na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali na UN-Habitat zinaendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali, ikiwamo usafiri endelevu na wa umeme, usimamizi wa taka, uchumi mzunguko, kupunguza taka za plastiki pamoja na kuboresha fursa za makazi, upatikanaji wa ardhi na mipango ya ukuaji wa miji. Amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha ukuaji wa miji unakuwa chachu ya ajira, uwekezaji, ulinzi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi” amesema Dkt.Lubaale.

Aidha, amesema kupitia mkakati wa mwaka 2026–2030, Serikali na UN-Habitat zinalenga kuimarisha mfumo jumuishi wa maendeleo endelevu ya mijini unaozingatia makazi ya gharama nafuu, usimamizi wa ardhi, uboreshaji wa makazi, usafiri endelevu na matumizi ya takwimu katika kupanga miji.

Amewataka wadau wote, wakiwamo wanawake, vijana, sekta binafsi, wataalamu na jamii, kushiriki katika mchakato huo ili kujenga miji yenye makazi bora, salama na himilivu, bila kumuacha mtu nyuma.

No comments:

SERIKALI YATAKA MAKAZI YAENDANE NA KASI YA UKUAJI WA MIJI

  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 2026 yal...